2014-11-17 09:04:36

Jengeni utamaduni wa watu kukutana na wala si kupigana!


Baba Mtakatifu Francisko mara tu baada ya tafakari ya Sala ya Malaika a Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu mjini Vatican, Jumapili tarehe 16 Novemba 2014, aliyaelekeza mawazo yake mjini Roma ambako kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na mgogoro mkubwa kati ya wahamiaji na wenyeji, mambo yanayojitokeza katika miji mbali mbali Barani Ulaya, hasa katika maeneo yaliyoko pembezoni mwa miji; maeneo ambayo wakati mwingine yamesahaulika, na hivyo kuwa ni chanzo kikuu cha migogoro ya kijamii.

Baba Mtakatifu anawaalika viongozi katika ngazi mbali mbali kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kutafuta suluhu ya matatizo ya raia wao kabla mambo hayaharibika. Jumuiya za Kikristo zisaidie kujenga na kudumisha mazingira ambayo yatawasaidia watu kukutana na wala si kupigana. Wahamiaji na viongozi wa Serikali wanaweza kupata nafasi ya kuzungumza kwa pamoja katika maeneo ya Parokia. Jambo la msingi ni kutoruhusu kamwe kinzani na migongano ya kijamii ichukue nafasi ya majadiliano sanjari na kusikilizana kwa amani na utulivu, ili kupanga kwa pamoja mambo msingi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watu kwa kushirikishana!

Tarehe 16 Novemba 2014, ilikuwa ni Siku ya Kimataifa kwa ajili ya kuwakumbuka watu waliokumbwa na ajali barabarani. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana amewakumbuka na kuwaombea watu walioathirika kutokan ana ajali barabarani na kuwataka watu kuwa makini kwa kuheshimu sheria na kanuni za usalama barabarani.







All the contents on this site are copyrighted ©.