2014-11-15 08:43:55

Yaliyojiri huko Assis wakati wa mkutano mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia


Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI, hivi karibuni limehitimisha mkutano wake wa 67 uliokuwa unafanyika mjini Assisi, kwa kuwashukuru na kuwapongeza Mapadre wanaoendelea kujisadaka kwa hali na mali kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Familia ya Mungu nchini Italia.

Katika mkutano wao, Maaskofu wamechambua na kukazia umuhimu wa Kanisa kuendelea kutangaza Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo sanjari na kujikita katika majiundo makini kwa Mapadre, ili waweze kutekeleza dhamana na utume wao kwa ari na moyo mkuu zaidi, wakitambua kwamba, kwa sasa wanahamishwa na Mama Kanisa kuwa na mwelekeo mpana zaidi wa maisha ya kimissionari, ili kutoka kifua mbele, tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa, Habari Njema ya Wokovu.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limepembua tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, matatizo, changamoto na fursa zilizopo, ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kutangaza Injili ya Familia. Wameonesha mshikamano wa udugu na upendo kwa Wakristo wanaoteswa na kunyanyaswa huko Mashariki ya Kati, kiasi kwamba, wanalazimika kuzikimbia nchi zao ili kusalimisha maisha yao. Mshikamano huu, umeoneshwa na Baraza la Maaskofu kwa kundi la Maaskofu kutembelea huko Nchi Takatifu ili kujionea wenyewe hali halisi.

Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, pamoja na mambo mengine limejadili kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Watawa Duniani, utakaozinduliwa hapo tarehe 30 Novemba, 2014 Jumapili ya kwanza ya Kipindi cha Majilio na kufungwa rasmi tarehe 2 Februari, 2016 Siku kuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya Watawa Duniani.

Maaskofu wamefafanuliwa kuhusu maandalizi ya maadhimisho ya Kongamano la tano la Kikanisa Kitaifa litakalofanyika Jimboni Firenze kuanzia tarehe 9 hadi tarehe 13 Novemba 2015.

Maaskofu wamehabarishwa kuhusu maandalizi ya Onesho la Sanda Takatifu litakalofanyika Jimbo kuu la Torino kuanzia tarehe 19 Aprili hadi tarehe 24 Juni 2015. Maaskofu pia wameanza maandalizi kwa ajili ya kushiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, itakayoadhimishwa kuanzia tarehe 26 hadi 31 Julai 2016, Jimbo kuu la Crakovia, Poland.Mwishoni, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia limewaandikia Mapadre barua ya kuwashukuru, kuwapongeza na kuwahimiza katika maisha na utume wao wa Kipadre kwa ajili ya ustawi wa Kanisa la Kristo na maendeleo ya watu!







All the contents on this site are copyrighted ©.