Uhuru na demokrasia ni mambo msingi katika ustawi na maendeleo ya binadamu!
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Ijumaa tarehe 14 Novemba 2014 amekutana
na kuzungumza na Rais Milos Zeman wa Jamhuri ya Watu wa Czech; tukio ambalo limekazia
kwa namna ya pekee umuhimu wa kukuza na kudumisha uhuru na demokrasia, kwa kujikita
katika kuendeleza haki msingi, utu na heshima ya binadamu.
Kardinali Parolin,
yuko mjini Prague kuanzia tarehe 13 Novemba 2014 ili kushiriki katika maadhimisho
ya Jubilee ya Miaka 25 tangu Agnese Bohemia alipotangazwa kuwa Mtakatifu kunako tarehe
12 Novemba 1989, tukio ambalo pia ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 25 ya Mapinduzi
ya kisiasa yaliyokomesha utawala wa Kikomunisti nchini humo.
Viongozi hawa
wawili wamezungumzia kuhusu hija tatu za kichungaji zilizofanywa na Mtakatifu Yohane
Paulo II pamoja na Baba Mtakatifu Benedikto XVI kunako mwaka 2009 pamoja na kuonesha
matumaini kuwa, panapo majaliwa, Baba Mtakatifu Francisko anaweza pia kutembelea nchini
humo, ili kujionea utajiri mkubwa wa maisha ya watu kiroho na kitamaduni. Baba Mtakatifu
Francisko atakuwa na furaha, ikiwa kama Rais Zeman atamtembelea mjini Vatican panapo
majaliwa.
Kardinali Parolin, akiwa nchini humo amepata fursa ya kuzungumza
na viongozi wakuu kwa kuonesha mchango wa Kanisa katika ustawi na maendeleo ya wananchi,
changamoto kwa sasa ni kukuza na kudumisha misingi ya uhuru na demokrasia ya kweli.
Hii ni nchi ya Watakatifu Cyril na Metodi; nchi yenye utajiri wa tunu msingi za maisha
ya kimaadili, kiroho na kitamaduni. Kanisa litaendelea kushikamana na wananchi wote
kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi, lakini zaidi kwa kuonesha mshikamano na
maskini pamoja na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, kwa kuwekeza katika sekta
ya elimu, afya na maendeleo endelevu.
Kardinali Parolin amekutana na kuzungumza
pia na wanadiplomasia wanaofanya kazi zao nchini Czech pamoja na kuwakumbuka Wakristo
wengi waliojisadaka maisha yao kwa ajili ya kupandikiza mbegu ya Ukristo na leo hii
Ukristo umeota mizizi na kukomaa licha ya madhulumu na nyanyaso zilizofanywa wakati
wa utawala wa Kikomunisti dhidi ya Kanisa. Kardinali Frantisek Tomasek, Askofu mkuu
wa Jimbo kuu la Prague, atakumbukwa na wengi kutokana na kusimama kidete kulinda na
kutetea imani kwa Kristo na Kanisa lake.
Baada ya kuanguka kwa Ukomunisti,
Czech ilianzisha uhusiano wa Kidiplomasia na Vatican, leo hii Kanisa linasonga mbele
katika mchakato wa kuwahudumia wananchi wa Czech, kwa kukazia utu na heshima ya binadamu,
haki, amani na upatanisho wa kitaifa.