Wizara ya afya, shirikianeni na sekta binafsi katika kutoa huduma bora kwa Watanzania!
Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda ameitaka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii nchini
Tanzania ipanue wigo wa utoaji huduma za msingi kwa kuishirikisha zaidi sekta binafsi
nchini. “Ninawasihi Waziri wa Afya na Naibu wake kwa vile ni wapya bado wabadili mtizamo
wa wizara hii kwa kushirikisha zaidi wadau wa sekta binafsi kwenye utoaji wa huduma
ili wasaidie kupunguza mzigo mkubwa ilionao Serikali,” alisema. Ametoa kauli hiyo
Ijumaa, Novemba 14, 2014 wakati akifungua Mkutano wa wa Kwanza wa Kitaifa wa Sekta
ya Afya wa mwaka 2014 ulioanza Ijumaa kwenye ukumbi wa mikutano wa kimataifa wa Mwalimu
Nyerere, jijini Dar es Salaam. Waziri Mkuu ambaye amefungua mkutano huo kwa niaba
ya Rais Jakaya Kikwete aliyeko nje ya nchi kwa matibabu alisema: “Kuna tatizo la kukumbatia
utoaji wa huduma ... tunazo hospitali kubwa za wilaya zinazomilikiwa na taasisi za
dini. Hivi ni kwa nini kama Wizara msiwasaidie kuwahudumia watumishi wao au kuwapa
ruzuku kwenye dawa ili kuwawezesha kutoa huduma kwa ufanisi zaidi?,” alihoji Waziri
Mkuu na kushangiliwa na washiriki wa mkutano huo. “Hata ukiangalia takwimu kwenye
utoaji wa huduma za afya kupitia mifumo ya bima ya afya utabaini kuwa ni asilimia
18 tu wananchi wanatumia bima ya afya na kati ya hao, asilimia 15.3 ni mifuko ambayo
imeanzishwa na Serikali. Ni kwa nini basi msiwasaidie wadau wa sekta binafsi ili wachangie
huduma hii na idadi wa watumiaji wa mfumo huu iongezeke haraka?,” alihoji. Akizumgumzia
kuhusu uwiano kati ya daktari na mgonjwa, Waziri Mkuu alisema uwiano uliopo ni mbaya
na kwamba hakuna njia ya haraka ya kupunguza tatizo hilo isipokuwa kwa kuishirikisha
sekta binafsi kwenye ujenzi wa vyuo vikuu vya elimu ya tiba na sayansi za jamii. “Uwiano
wa sasa hapa nchini ni daktari mmoja kwa wagonjwa 75,000 wakati viwango vya kimataifa
vinataka daktari mmoja awahudumie wagonjwa 7,000. Kwa wauguzi, hapa nchini muuguzi
mmoja anahudumia wagonjwa 6,000 wakati viwango vya kimataifa vinataka muuguzi mmoja
ahudumie wagonjwa 500,” alisema. “Kwa uwioano huu safari bado ni ndefu. Tunapaswa
tuangalie tutafanyaje ili watu binafsi waje kuwekeza kwenye elimu ya juu ya sayansi
na tiba, wajenge vyuo vya tiba, wajenge hospitali kubwa, na sisi pia kwa upande wa
Serikali ni lazima tuseme tunawapa vivutio gani hawa wawekezaji hadi wakubali kuwekeza
kwenye eneo hilo,” alisema. “Tunataka mkutano huo uje na mapendekezo ambayo mnataka
Serikali iyafanyie kazi na hatimaye isaidie kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa
wananchi,” alisema Waziri Mkuu. Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya
kufungua mkutano huo, Waziri Mkuu alisema Serikali inaendelea kudhibiti ugonjwa wa
ebola kwenye vituo vya mipakani na kwenye viwanja wa ndege. “Mpaka sasa hatujapata
kesi ya ugonjwa wa Ebola hapa nchini... changamoto kubwa ni ukubwa wa mipaka yetu.
Si wageni wote wanaoingia nchini wanapita kwenye vituo rasmi, wapo wanaotumia njia
za vichochoroni. Rai yangu ni kuwaomba Watanzania wawe waangalifu kutambua ni wageni
gani wanaingia kwenye maeneo wanayoishi,” alisema. Mkutano huo wa siku mbili unamalizika
Jumamosi, Novemba 15, 2014.