Wananchi Barani Afrika wanapaswa kujifunga kibwebwe kwa ajili ya maendeleo yao!
Kardinali Peter Turkson, Rais wa Baraza la Kipapa la haki na amani amewataka wananchi
Barani Afrika kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika
mchakato wa maboresho ya maisha ya watu wa Bara la Afrika, vinginevyo, Jumuiya ya
Kimataifa itakuwa inabuni na kupanga mikakati ambayo haiwezi kuzaa matunda yanayokusudiwa.
Umefika wakati kwa Bara la Afrika kuwa na mwono mpana zaidi kuhusu mikakati inayoweza
kuleta mabadiliko ya kweli kwa wananchi wa Bara la Afrika.
Kardinali Turkson
ameyasema haya hivi karibuni alipokuwa anazungumza na wajumbe waliokuwa wanashiriki
katika semina ya siku tatu iliyoandaliwa na Chuo Kikuu cha Tangaza, kilichoko, Nairobi,
Kenya, iliyokuwa inapania pamoja na mambo mengine kuangalia mbinu mkakati na miundo
inayoweza kuleta mabadiliko Barani Afrika kwa kuvishirikisha vyama vya kitume katika
mchakato wa maendeleo endelevu.
Kardinali Turkson amesema, NEPAD ilikuwa na
mwono na mipango kamambe kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika, lakini
kwa bahati mbaya NEPAD haikujiamini wala kuonesha utashi wa kutekeleza mwono huu katika
uhalisia wa maisha ya wananchi wa Bara la Afrika. Umoja wa Afrika kwa sasa unajitahidi
kuokota makapi ya mipango na mikakati iliyoshindwa kutekelezwa na NEPAD kwa ajili
ya ustawi na maendeleo ya Bara la Afrika.
Vyama vya kitume vinaweza kusaidia
kuchochea maendeleo ya wananchi wa Bara la Afrika, lakini ifahamike kwamba, hili ni
jukumu la kwanza kabisa ambalo linapaswa kutekelezwa na viongozi wa Serikali na wanasiasa.
Kuna ndoto nyingi ambazo zinajikita katika mchakato wa mabadiliko ya kijamii Barani
Afrika, lakini ndoto bila kutekelezwa zinabaki kuwa ni ndoto tu! Huu ni mchakato ambao
wananchi wa Afrika hawana budi kushiriki kikamilifu, vinginevyo, mipango ya maendeleo
itaendelea kubaki kwenye makaratasi.
Naye Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti
wa Tume ya haki na amani Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya amekiri mchango wa Kanisa
katika mchakato wa kuandika Katiba mpya kunako mwaka 2010, ili kukoleza maendeleo
ya watu nchini Kenya. Lengo ni kumwendeleza mtu mzima: kiroho na kimwili, kwa kulinda
na kudumisha utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Vyama
vya kitume na Taasisi mbali nchini Kenya vilichangia katika kukuza na kuimarisha ukweli
na uwazi.