2014-11-13 09:01:23

Kazi yako ndilo jina lako!


Katika barua kwa Wagalatia na Warumi, Mtume Paulo anasema wokovu wetu, yaani uhusiano wetu na Mungu, huja si kwa matendo yetu bali kwa imani. Hapa hatuna budi kujua kwamba kwa matendo Mtume Paulo anamaanisha kuwa ni yale yanayooneshwa au kuorodheshwa katika sheria ya Musa na pia ana maana matendo ambayo hutendwa tu kwa mtazamo wa kibinadamu.

Tujue pia kuwa Mtume Paulo akiongea kuhusu wokovu katika – Gal. 2:16 –anasema hivi: lakini kwa kuwa tumetambua ya kuwa mwanadamu hafanywi mwadilifu kwa matendo ya sheria ila kwa kumwamini Yesu Kristo, nasi tumemwammini Yesu Kristo tupate kuthibitishwa kwa kumwamini Kristo, si kwa matendo ya sheria. Hapa yaaonekana Paulo akitaja imani tu kama inatosha kupata wokovu.

Akiongea juu ya wokovu kwa imani anamaanisha kujikabidhi kwa Mungu, kutoa nafasi kwa pendo lake ambalo humiminwa kwetu. Hakuna awezaye kulazimisha pendo la Mungu. Ni Mungu anayekuja kwetu.. Mtume Yohani anaweka wazi uelewa huu – 1 Yoh: 4:16 – nasi tumejua mapendo anayotuelekeza Mungu, tukayaamini. Mungu ni upendo, na mwenye kuishi katika upendo, anaishi ndani ya Mungu na Mungu anaishi ndani yake. Kwamba Mungu ni upendo, hivyo ni lazima apende, hatuwezi kumbadilisha.

Lakini Mtume Paulo anayesema tutafanywa wenye haki kwa imani katika Yesu katika Wagalatia 2:16 anafafanua mafundisho yake katika Rum. 2:6 – akisema atamlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake na katika Rum. 2:13 – anasema – si wenye kuisikia sheria walio waadilifu kwa Mungu, bali wenye kuitimiza sheria ndio watakaofanywa waadilifu.

Ni kwa njia ya zawadi ya imani, tuko wake, tunaishi kwake na tu mali yake. Katika Gal. 2:20 tunasoma – si mimi tena ninayeishi, bali ni Kristo anayeishi ndani yangu. Muda ninaoishi bado mwilini, ninaishi katika imani inayomtegemea Mwana wa Mungu, ambaye amenipenda na kujitoa kwa ajili yangu. Hapa tunawajibishwa kwa kile alichotujalia Mwenyezi Mungu na masomo yetu ya leo na hasa Injili inatudai kutenda, kufanyia kazi ile talanta aliyotujalia Mungu na ya kwanza kati ya hizo ikiwa ni IMANI.

Sisi hatuna budi kutenda mema. Mtakatifu Gaspar del Bufalo, Mwanzilishi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu anasema kwa Mungu ni lazima kutenda mengi,- kwa sababu mambo ya Mungu ni mengi, haraka – kwa sababu maisha yetu ni mafupi na vizuri – kwa sababu ndivyo inavyompendeza Mungu. Hivyo matendo mema yanahitajika. Matendo hayo mema ni majibu yetu kwa upendo na maisha mapya katika Kristo. Mtume Paulo katika – Rom. 2:13 – si wenye kuisikia sheria walio waadilifu kwa Mungu, bali wenye kuitimiza sheria ndio watakaofanywa waadilifu.

Mcheza kamari mmoja alimkasirikia Mungu kwa kutokushinda bahati nasibu. Alishika tangazo lililomwalika na kumkumbusha uwepo wa bahati nasibu hiyo. Akaanza kusali. Hakutaka kununua tiketi za ushiriki. Alipokosa, akamlaumu Mungu kuwa hakusikia sala na maombi yake.

Tumesikia katika masomo yetu:
    sifa za mwanamke Mwisraeli – mchapa kazi, mwema, mtu wa sala ambaye kazi zake humletea sifa. Kazi zake zinasifia utu wake na jina lake. Mchora picha maarufu Mwitaliano – Michelangelo – aliona pande la jiwe katika shamba la mkulima mmoja, akamwomba jiwe hilo. Yule mkulima akampatia mara moja akisema kwamba halina thamani ye yote. Michelangelo akasema nipatie mimi kwani ndani yake amefungwa malaika, nataka nimweke huru. Falsafa inasema kazi yako ni jina lako.


    Huku tukisubiri ujio wa Kristo, ni lazima tuishi maisha ya Kikristo, katika mwanga, huku tukitenda matendo ya mwanga.


    Zile talanta – ni kitu kipya, ndiyo zawadi ya Mungu - IMANI, ndiyo maisha mapya –zawadi toka kwake. Ni lazima kutunza na kukuza zawadi hizo. Hii ndiyo namna ya kupata wokovu.


Mtoto mmoja alimsubiri babaye kutoka kazini usiku wa manane. Baba yake alishangaa kumkuta mwanae mdogo bado akiwa macho usiku ule. Baada ya kusalimiana yule mtoto akamwuliza baba yake – eti baba huwa unalipwa shilingi ngapi kila saa moja ya kazi unayofanya? Baada ya mshangao na hata kumwambia kuwa hata mama yako hajui yule mtoto alisisitiza kupata jibu. Baba hakuwa tayari kumwambia ila baada ya tafakari ya kina, alimfuata mwanaye chumbani na kumwambia huwa nalipwa elfu ishirini kwa saa. Yule mtoto akainua mto wake akatoa kiasi hicho cha fedha akampatia baba yake. Akamwomba amlipe saa moja ya kazi ili huo muda autumie kukaa naye nyumbani. Huyu mtoto alitamani kupata mapenzi ya baba yake. Huyu baba alitumia maisha yake yote kufanya kazi kwa bidii ajili ya familia. Ila hakuwa na muda na familia yake. Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu Kristo – ana sifa ya mfanyakazi bora. Tuige mfano wake.

Hatuna budi kuangalia tena leo jinsi tunavyoishi imani yetu kwa matendo. Hatari kubwa ni kuwa kama yule mtumwa aliyepewa talanta moja. Wengi wetu hatutumii vilivyo vipaji alivyotujalia Mungu. Leo hii kila mmoja wetu atafakari na kujiuliza aliyojaliwa na Mungu na jinsi anavyomrudushia Mungu. Pengine kwa Mungu tunafanya kidogo mno. Matendo yetu ya kila siku yanaakisi imani yetu au tumetenganisha imani na matendo?

Leo tunaalikwa kufanyia kazi vipaji/talanta alizotujalia Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu Francisko daima anaalika Wakristo kutoka na kwenda kwa maskini na wenye mahitaji zaidi yetu. Anatualika kufanya kitu. Hapa inaonekana wazi kuwa ni lazima kutenda, kufanya kitu. Ni wajibu wetu tunaomwamini Mungu. Yule anayempenda Mungu na kumwamini anaalikwa kwenda kupeleka ujumbe wa Neno la Mungu kwa wengine. Hapa ndipo ilipo changamoto kubwa. Je tunafanya kitu? Kwa kiasi gani na namna gani?

Mtu haokolewi kwa kazi lakini pia huokolewa kwa kazi– yaani matendo yake mema – by F.J. LEENHARDT. Naye Booker T. Washington anasema – mafanikio hayapimwi sana kwa nafasi aliyofikia mtu katika maisha, bali kwa jinsi alivyokabiliana na vikwazo katika harakati za kujaribu kufaulu. Hapa dhama ya kufanya kitu inajirudia tena. Imetayarishwa na Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.