Kufutwa au kuendelea kuwepo kwa adhabu ya kifo ni kati ya mada tete zinazojadiliwa
na Bunge la Zimbabwe kwa wakati huu, kwani Zimbabwe ni kati ya nchi chache duniani
ambazo zina adhabu ya kifo. Takwimu zinaonesha kwamba, tangu kunako mwaka 2004 adhabu
ya kifo haijawahi kutekelezwa nchini Zimbabwe.
Bado kuna vuta ni kuvute ya
kutaka kuendelea au kusitisha adhabu ya kifo inayoungwa mkono na Mwanasheria mkuu
wa Zimbabwe Bwana Johanes Tomana, lakini anapingwa na Waziri wa sheria Bwana Emmerson
Mnangagwa, moja ya wasaidizi wa karibu sana na Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe! Wachunguzi
wa mambo wanasema, pengine Waziri huyu akamrithi Rais Mugabe!
Kanisa Katoliki
linafundisha kwamba, maisha ya binadamu ni kitu kitakatifu kwani tangu mwanzo wake
kinahusiana na kazi ya Mwenyezi Mungu ya kumuumba mwanadamu na hivyo kuwa na mahusiano
ya pekee kabisa na binadamu, aliye peke yake kikomo chake. Mwenyezi Mungu peke yake
ndiye asili ya uhai na hatima yake. Hakuna mazingira yoyote yanayoweza kujitwalia
haki ya kuharibu moja kwa moja uhai wa binadamu. Watu wengi wanasema, adhabu ya kifo
imepitwa na wakati.