2014-11-12 08:11:56

Zingatieni: udugu, sala na utume katika majiundo yenu ya Kipadre!


Udugu, maisha ya sala, utume na maisha ya Kanisa ni mambo msingi kwa Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya maisha ya Kipadre ndani ya Kanisa. Ni wosia uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa Majandokasisi kutoka Ufaransa waliokuwa wanafanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, Ufaransa kuanzaia tarehe 8 hadi 10 Novemba 2014. Hii ni hija ambayo imewashirikisha Majandokasisi 750 wanaoendelea kufundwa kwa ajili ya maisha ya Kipadre nchini Ufaransa.

Baba Mtakatifu anawataka Majandokasisi kujenga na kudumisha umoja na mshikamano katika maisha na utume wao, wakijitahidi kumwilisha Ujumbe wa Injili katika uhalisia wa maisha, kama kielelezo cha ushuhuda wa utume wao kwa Kristo na Kanisa lake, kwa kuweka kando ubinafsi. Seminari pawe ni mahali pa kuishi kwa umoja, upendo na mshikamano; mahali pa kufahamiana na kusaidiana kwa hali na mali pamoja na kuonesha ushuhuda wa pamoja wa neema inayobubujika kutoka kwa wafuasi wa Kristo wanaojisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Majandokasisi kukua na kukomaa katika upendo na mshikamano wa kidugu pamoja na kuendelea kumtumainia Roho Mtakatifu, ili hatimaye, watakapofikia Daraja Takatifu la Upadre, Udugu liwe ni neno ambalo ni sehemu ya vinasaba vya maisha yao ya kila siku. Majandokasisi wawe ni watu wa sala na tafakari ya kina kama walivyofanya Mitume pamoja na Bikira Maria walipokuwa wamekutanika kwenye Chumba cha juu, huku wakisubiri zawadi ya Roho Mtakatifu.

Neno la Mungu liwe ni taa na mwanga katika maisha yao na kwamba, Sala daima inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha. Majandokasisi wajitahidi kutumia vyema muda wao kwa ajili ya Sala, tafakari na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kweli Yesu mwenyewe aweze kuzima kiu ya maisha yao ya ndani. Majandokasisi wajifunze kusali kwa unyenyekevu, ili kumwachia nafasi Mwenyezi Mungu aweze kuwafunda kadiri ya mapenzi yake na kuwa kweli ni "Watu wa Mungu".

Baba Mtakatifu anawakumbusha Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya kupokea Daraja takatifu la Upadre kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanashiriki dhamana ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu. Watakapopewa Daraja Takatifu, watakabidhiwa na Maaskofu wao dhamana kubwa zaidi ya kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa, kwa kuwagawia watu Mafumbo ya Kanisa.

Hapa watakuwa wanatekeleza amri ya Kristo ya kwenda ulimwenguni kote ili kuwafanya wote kuwa ni wafuasi wake, huku wakiwabatiza katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Hapa Majandokasisi wanapaswa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu wenye mvuto na mguso katika maisha na utume wa Kimissionari.

Baba Mtakatifu kwa namna ya pekee, anawasihi vijana kujitahidi kuufahamu ulimwengu, mahali watakapokutana na watu, wajitahidi kuwatakatifuza kwa njia ya mifano bora ya maisha yao, hasa kwa kuwaendea wale ambao kwa muda mrefu wamesahau mahali ambapo kuna mlango wa Kanisa. Wajitahidi kuwaendelea watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii bila ya kuwasahau wale ambao wako mijini, kwa kutambua kwamba, utume wa Kanisa unafumbatwa katika maisha ya sala, ili kuwa kweli ni wahudumu waaminifu wa Mafumbo ya Kanisa kwa Familia ya Mungu.

Baba Mtakatifu anawakumbusha Majandokasisi kwamba, Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa katika hija ya maisha yake hapa duniani alijitahidi kumsindikiza Mwanaye wa pekee katika hatua mbali mbali za maisha na utume wake, hadi aliposimama pale chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye! Bikira Maria awasindikize Majandokasisi katika maisha na majiundo yao, ili kweli waweze kuwa ni wachungaji wema na watakatifu kadiri ya mpango wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.