2014-11-12 07:13:02

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Tunakualika katika tafakari yetu ya Dominika ya 33 ya mwaka A wa Kanisa, Habari Njema ikiwa mwaliko wa kuwa tayari na wakati huo tukitumia vema na pasipo kuogopa talanta au karama tulizokabidhiwa na Mungu kwa mafaa ya Jumuiya na kwa safari ya wokovu. RealAudioMP3

Mpendwa mwana wa Mungu, katika somo la kwanza toka kitabu cha Mithali tunasikia habari ya mke mwema ambaye ajitahidi kutumia talanta alizopewa kumpendeza mmewe na hivi moyo wa mmewe humwelekea na kumpenda kwa uaminifu na kumtendea mema. Mwanamke huyu ni mkarimu, huwatazama maskini na kuwapa mahitaji yao. Mwanamke huyu ni mcha Mungu, hushika amri za Mungu na hivi husifiwa!

Mwandishi wa somo la kwanza ametumia mfano wa mwanamke ampendezaye mmewe kuelezea wajibu wa taifa la Israeli jinsi linavyopaswa kutumia talanta ya upendo yaani kumpenda Bwana na mapato ya upendo yakiwa ni kujipatia wokovu. Wajibu huu wa taifa la Israeli sasa tunao sisi wana wa kanisa la leo tukiitwa kujibu upendo wa Mungu ambao watujia kila dakika ya maisha yetu.

Tunapaswa kuujibu kwa kujenga uaminifu wa kiinjili, ambao hutualika kushika vema wito wa ubatizo wetu katika kutangaza daima matendo makuu ya Mungu kwa mataifa, ndiyo umisionari, ndiyo matumizi ya talanta tulizopewa na Mungu.

Katika somo la pili mtume Paulo kwa Watesalonike, anahimiza uaminifu kwa ubatizo wetu na injili badala ya kubaki katika kuulizauliza lini Bwana atakuja mara ya pili. Anawakumbusha kuwa Bwana atakuja saa ambayo sisi sote hatutambui, hata hivyo kwa kuwa tumepokea ubatizo na injili na hivi hatuko gizani tena siku hiyo haipaswi kuwa ya kutushitukiza bali siku ya heri ya kumlaki Bwana anayekuja katika nuru. Kwa namna ya kukesha na kuwa na kiasi katika yote ili roho zetu zijazwe na neema nyingi, Bwana atatukuta tu tayari.

Mwinjili Mathayo anatuwekea fundisho kuhusu wajibu wa kukesha tukitumia talanta tulizopewa na Mungu kwa uaminifu na zaidi kuweza kuzaa matunda. Fundisho hili lina mizizi katika mambo matatu, jambo la kwanza ni lile la kuwa, kila mmoja wetu amepewa talanta kadiri ya uwezo wake na jambo la pili ni lile kwamba kila mmoja anapaswa kuzalisha kadiri alivyopewa.

Jambo la tatu lahusu kulimbikiza pasipo kutumia talanta na hivi jambo hili ni kinyume cha aliyetoa talanta hizo na mwishoni ni kunyanganywa. Pamoja na kunyanganywa yeye mwenyewe kutupwa katika giza la nje ambako kutakuwa na kilio na kusaga meno! Mpendwa tunaweza kusema kwa kifupi kuwa tunaalikwa kuwa tayari kila saa tukitumia talanta tulizopewa, tukisubiri ujio wa Bwana atakayekuja.

Talanta ambazo Bwana amekabidhi wakati wa pasaka ni Habari njema, sakramenti, uwezo wa kuponya, upendo kwa maskini na yote mema kwa ajili ya wokovu. Hazina hizi ziko katika jumuiya ya kikristu na hivi jumuiya inapaswa kuzikuza ili ziweze kuzaa matunda kwa ajili ya wokovu wa watu. Kumbe kama mmoja anatangaza Neno la Mungu yampasa kwanza kulielewa, kulitafsiri kadiri ya mazingira ya watu wa sasa na kulitangaza likigusa mazingira halisia. Tena yafaa kukumbuka kuwa, Neno la Mungu linakata na hivi hapana haja ya kuogopa kwamba litamwumiza mmojawapo wa wapokeaji wa neno hilo. Lazima Neno la Mungu liguse mioyo ya watu, na kwa namna hiyo linabadilisha mtizamo na kuzaa matunda.

Mpendwa msikilizaji, kutotumia talanta ni kuinyonya jumuiya, kwa maana jumuiya daima hutegemea kupata faida kwa maendeleo yake. Kwa sababu hiyo basi lazima mmoja anyanganywe na kupewa mwingine atakayetoa faida mwishoni mwa muda aliopewa. Katika safari ya wokovu muda wa talanta kuzaa matunda ni tangu pasaka mpaka ujio wa pili wa Bwana. Kwa hivi basi mwana wa Mungu kumbuka unayo nafasi tele tangu sasa hujachelewa, weka talanta zako katika safari ya wokovu, wajibika ili Bwana akukute uko macho na tayari katika NEEMA YA UTAKASO. Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.