Siku ya 5 Kimataifa ya kupambana na homa ya mapafu!
Shirika la kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF, katika maadhimisho ya Siku
ya Tano ya Kimataifa ya kupambana na Ugonjwa wa Homa ya Mapafu, inayoadhimishwa kila
mwaka ifikapo tarehe 12 Novemba, linasema kwamba, idadi ya watoto wanaofariki dunia
kutokana na ugonjwa wa homa ya mapafu imepungua kwa asilimia 44%, ingawa bado Jumuiya
ya Kimataifa inapaswa kujizatiti zaidi, kwani watoto chini ya umri wa miaka mitano
wanaendelea kupoteza maisha yao kwa magonjwa yanayoweza kuzuilika!
Mickey
Chopra, Mkurugenzi wa afya ya umma UNICEF anasema, hata hivyo hakuna sababu kwa Jumuiya
ya Kimataifa kujipongeza kwa hatua hii iliyofikiwa kwani kuna watoto wanaoendelea
kuteseka kutokana na umaskini, njaa na utapiamlo. Kumbe, jitihada za kuokoa maisha
ya watoto hazina budi kuwafikia watoto wengi zaidi kwa kupambana na magonjwa yanayosababisha
vifo vya watoto wadogo, kwa kukazia chanjo, uchunguzi wa magonjwa pamoja na tiba makini.
UNICEF
inawataka wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba, wanaendeleza tafiti
zinazopania kupambana na hatimaye, kutokomeza ugonjwa wa homa ya mapafu kwa kuhakikisha
kwamba, watu wanapata dawa bora kwa bei nafuu.