2014-11-12 07:29:11

Dumisheni umoja wa kitaifa na amani Zambia!


Askofu mkuu Telesphore Mpundu wa Jimbo kuu la Lusaka, Zambia wakati wa Ibada ya mazishi ya Rais Michael Chilufya Sata yaliyohudhuriwa na umati mkubwa wa wananchi kutoka ndani na nje ya Zambia, Jumanne tarehe 11 Novemba 2014, amewataka wanasiasa nchini Zambia kuhakikisha kwamba wanadumisha na kukuza umoja na mshikamano wa kitaifa, hasa wakati wa kampeni za kuwania kiti cha Urais.

Ni wajibu wa Serikali ya mpito kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu unakuwa: huru, haki na uwazi, ili kuwawezesha wananchi wa Zambia kutekeleza wajibu wao wa kikatiba.

Rais Sata aliyefariki dunia huko London, Uingereza tarehe 28 Oktoba 2014 amezikwa kwenye Uwanja wa Mabalozi mjini Lusaka na umati mkubwa wa waombolezaji wamefuatilia tukio hili kwa simanzi na majonzi makuu. Askofu mkuu Mpundu amewataka wanasiasa kuiga mfano bora wa Marehemu Rais Sata ambaye katika chaguzi mbali mbali nchini Zambia alishindwa mara tatu, lakini hakukata tamaa wala kuingia "porini" kutafuta madaraka kwa matumizi ya nguvu. Wakati wa kampeni, wanasiasa wauze sera na mikakati inayopania kuwaletea wananchi wa Zambia ustawi na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Askofu mkuu Mpundu anasema, Zambia kwa sasa inahitaji mambo makuu mawili: mshikamano wa kitaifa na amani; mambo msingi yatakayowawezesha kupambana na umaskini wa hali na kipato, ili kuboresha maisha yao zaidi. Wanasiasa na vijana wajifunge kibwebwe ili kufanya kazi kwa tija na ufanisi mkubwa kwa ajili ya watu wao kabla ya kuanza kutamani madaraka makubwa!







All the contents on this site are copyrighted ©.