2014-11-11 11:14:38

Wekeni ubinafsi, uchu wa mali na madaraka pembeni; tafuteni kwanza mafao ya wengi!


Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anasema, umefika wakati kwa viongozi wa Serikali na kisiasa nchini Nigeria kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi, utu na heshima ya binadamu, badala ya mtindo wa sasa wa kukaa na kuangalia watu wakiendelea kupoteza maisha na mali zao, kwa kuhofia kupoteza kura wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka 2015.

Askofu mkuu Kaigama ambaye amerejea hivi karibuni kutoka London, Uingereza alikokuwa anahudhuria mkutano uliokuwa unajadili kuhusu uhuru wa kidini, anasema, inasikitisha kuona kwamba, kuna watu bado wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, ambacho kwa sasa kinatawala maeneo mengi yaliyoko Kaskazini mwa Nigeria, licha ya uwepo wa vikosi vya ulinzi na usalama.

Hii inaonekana kwamba, viongozi wa Serikali na kisiasa wanaelekeza nguvu zao zaidi katika kupanga mikakati ya kushinda uchaguzi mkuu mwaka 2015 na kusahau kwamba, kuna watu wanaendelea kupoteza maisha yao kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko Haram. Umefika wakati wa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao ya wengi na uzalendo badala ya kujikita katika ubinafsi, uchu wa mali na madaraka.







All the contents on this site are copyrighted ©.