Serikali ya Kenya kuunda timu kuchunguza madai kuhusu chanjo!
Wizara ya Afya nchini Kenya imeunda timu maalum itakayochunguza madai ya Baraza la
Maaskofu Katoliki Kenya kwamba, chanjo ya Pepopunda inayotolewa kwa sasa inataka kudhibiti
ongezeko la idadi ya watu nchini Kenya.
Timu ya uchunguzi inatarajiwa kuundwa
wakati wowote kuanzia sasa kutona na taarifa iliyotolewa na Bwana James Macharia,
Katibu mkuu wa Wizara ya Afya nchini Kenya. Wawakilishi kutoka Baraza la Maaskofu
Katoliki Kenya na Chama cha Madaktari Wakatoliki watashirikishwa katika timu hii ya
uchunguzi, ili kuweza kujiridhisha kwamba, chanjo inayotolewa kwa wananchi wa Kenya
haina madhara yoyote kwa maisha ya watu.
Serikali ya Kenya inasema kwamba,
chanjo inayotolewa haina madhara na badala yake, kuna makosa ya kutafsiri chanjo hii
yanayofanywa na Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya katika maabara zake. Uchunguzi utafanyika
kwa kuzingatia sayansi kwa kuwashirikisha wadau mbali mbali ili kupata ukweli wa mambo
kuhusu chanjo hii.
Maaskofu kwa upande wao wanasema, chanjo hii imechafuliwa
na homoni ijulikanayo kama "Beta-HCG" ambayo inaweza kusababisha utasa na uharibifu
mkubwa wa mimba. Chama cha Walimu wa shule za Msingi Kenya wameungana na Baraza la
Maaskofu Katoliki ili kuonesha wasi wasi wao kuhusu chanjo inayotolewa kwa wananchi
wa Kenya, kwa hofu kwamba, kama kweli ina madhara, basi, walimu wengi watakosa fursa
za ajira kwa siku za usoni, kwani hakutakuwepo na watoto wa kufundishwa tena!