2014-11-10 09:38:02

Vunjilieni mbali kuta zinazoendelea kutenga na kuwagawa watu!


Jumuiya ya Kimataifa hapo tarehe 9 Novemba 2014 imeadhimisha kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 25 tangu Ukuta wa Berlin ulipoangushwa na watu wakaandamana kwa amani na utulivu, changamoto ya kuvunjilia mbali kuta za utengano ambazo bado zinajionesha kati ya Korea ya Kaskazini na Korea ya Kusini; Kati ya Palestina na Israeli, Sudan Kongwe na Sudan ya Kusini pamoja na Visiwa vya Cyprus ambavyo bado vinaonesha ukakasi wa utengano kati ya watu.

Hii ni changamoto iliyotolewa na Dr. Olav Tveit Fyskse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wakati wa maadhimisho ya Ibada ya Neno la Mungu kwa ajili ya kumbu kumbu ya Jubilee ya miaka 25 tangu kuanguka kwa Ukuta wa Berlin. Mageuzi haya makubwa ya kihistoria ni mchango uliofanywa na waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema waliokuwa wanaombea misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu. Watu walitaka kuona haki, amani na utunzaji bora wa mazingira unazingatiwa.

Waamini na watu wote wenye mapenzi mema bado wanahimizwa na Baraza la Makanisa kufanya hija ya haki na amani, kama mwendelezo wa changamoto iliyotolewa kwenye Mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliofanyika huko Korea ya Kusini, mwaka 2013. Vijana wana sehemu kubwa katika mchakato wa kuleta mageuzi ndani ya jamii, lakini wanapaswa kuwa na mwono mpana zaidi unaozingatia tunu ya maisha, haki na amani.

Baraza la Makanisa Ulimwenguni linayapongeza Makanisa mbali mbali kwa kuhamasisha waamini kujiunga na kampeni juu ya utunzaji bora wa mazingira kama sehemu ya maandalizi ya mkutano wa Jumuiya ya Kimataifa utakaojadili kuhusu mazingira huko Paris, Ufaransa, mwaka 2015. Mataifa mengi bado yanayonesha ukuta mkubwa wa upinzani, lakini hata ukuta huu unaweza kuanguka kama ulivyoanguka ukuta wa Berlin, ulioonesha chuki na uhasama wa kisiasa.

Baraza la Makanisa Ulimwengu linasema, matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii ni njia makini ya kulijengea Kanisa uwezo wa kutetea misingi ya haki na amani, kwani hapa watu wanaweza kushirikishana uzoefu na mang'amuzi yanayogusa maisha ya watu, ili kwa pamoja kuchukua hatua msingi katika maboresho na utunzaji bora wa mazingira.







All the contents on this site are copyrighted ©.