2014-11-10 07:38:55

Utawala wa sheria ulinde na kudumisha usawa kati ya watu!


Umoja wa Mataifa umejengeka katika msingi wa amani na usalama wa kimataifa; haki msingi za binadamu na maendeleo ya binadamu, mambo muhimu sana katika kukuza na kuendeleza utawala wa sheria unaothamini pia utu na heshima ya binadamu kama kielelezo cha kanuni maadili. RealAudioMP3

Utawala wa sheria hauna budi kujielekeza kulinda na kudumisha usawa kati ya watu wa mataifa, sheria za kimataifa, mikataba na itifaki zilizoridhiwa na Jumuiya ya Kimataifa; mambo msingi yanayopania kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa kujikita katika mafao ya wengi.

Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akichangia hoja kwenye mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, uliokuwa unajadili hivi karibuni kuhusu utawala wa sheria, anasema binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza pamoja na kuendelea kukazia miundo mbinu ya utekelezaji wa sheria. Uaminifu wa kijamii, mshikamano, uwajibikaji wa jamii husika, utawala bora na elimu maadili ni mambo muhimu katika kukuza na kudumisha utawala wa sheria, unaozingatia maendeleo ya mtu mzima. Tamko la haki msingi za binadamu ni dira na mwongozo unaopaswa kufuatwa na kutekelezwa na Jumuiya ya Kimataifa kama kielelezo cha haki ndani ya Jamii.

Jumuiya ya Kimataifa inayo wajibu wa kulinda na kudumisha uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu pamoja na utambulisho wa watu mahalia. Kinzani za kivita zinazoendelea huko Mashariki ya Kati na sehemu mbali mbali za dunia zinahitaji kupatiwa jibu makini kwa kuzingatia utawala wa sheria. Jumuiya ya Kimataifa inawajibika kulinda haki na usawa unaojikita katika utambuzi wa utu wa mwanadamu na haki zake msingi.

Ni matumaini ya Vatican kwamba, ongezeko la vitendo vya kigaidi, dhuluma na nyanyaso zinazojikita katika masuala ya kidini, iwe ni fursa kwa Jumuiya ya Kimataifa kuimarisha utawala wa sheria kwa kujikita katika uwajibikaji wa pamoja, ili kulinda na kuwatetea watu dhidi ya dhuluma na nyanyaso wanazokabiliana nazo kwa sasa.








All the contents on this site are copyrighted ©.