Marehemu Rais Sata, "King Cobra" atakumbukwa na wengi!
Rais Michael Chilufya Sata wa Zambia aliyefariki dunia kunako tarehe 28 Oktoba 2014
huko London Uingereza anazikwa tarehe 11 Novemba 2014 kwenye Makaburi ya Taifa yaliyoko
kwenye Uwanja wa Mabalozi, mjini Lusaka. Mazishi haya yatatanguliwa na Ibada ya Misa
takatifu, itakayoadhimishwa kwenye Uwanja wa Mashujaa wa Zambia na baadaye maziko
yatafuatia.
Katika kipindi cha majuma mawili ya maombolezo wananchi wa Zambia
pamoja na watu wenye mapenzi mema wamemkumbuka kwa sala na ibada mbali mbali, ili
kumwombea pumziko la uzima wa milele. Wananchi wa Zambia wanaoishi mjini Roma na katika
viunga vyake, Jumapili tarehe 9 Novemba 2014 wameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu
kwa ajili ya kumwombea Marehemu Rais Sata wa Zambia, aliyefahamika na wengi kama "King
Cobra".
Ibada hii ya Misa takatifu imeongozwa na Padre Paul Samasumo, Mkuu
wa Idara ya Kiingereza ya Radio Vatican aliyefafanua kuhusu Fumbo la Kifo katika maisha
ya mwanadamu, akiwataka waamini na watu wenye mapenzi mema waliohudhuria katika Ibada
hii ya Misa Takatifu kujiandaa kikamilifu ili kukabiliana na Fumbo la Kifo, kwani
hawajui siku wala saa watakapokutana na kifo. Lakini jambo la msingi ni kuhakikisha
kwamba, walau wanakumbukwa.
Padre Samasumo anasema, Marehemu Rais Sata atakumbukwa
na wengi kwamba alikuwa ni mchapakazi, mzalendo na mnyenyekevu, mtu aliyekubali kushindwa
na kusonga mbele kwa imani na matumaini. Hakuwa ni mtu aliyetaka kung'ang'ania madaraka
hata kwa gharama ya maisha ya wananchi wa Zambia. Amewataka wananchi wa Zambia kuendelea
kusali kwa ajili ya amani na utulivu wakati huu wa kipindi cha mabadiliko kuelekea
uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika katika kipindi cha siku tisini.
Rais
Guy Scott anasema, angependa kukumbukwa kwamba, ameiongoza Zambia kwa amani na utulivu
na kufanikisha mchakato wa uchaguzi mkuu kadiri ya Katiba ya nchi na wala si vinginevyo.