Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya limeitaka Serikali kuchukua maamuzi machungu kwa
kufanya mabadiliko makubwa katika vyombo vya ulinzi na usalama baada ya askari 20
kuuwawa kikatili na kikundi cha majambazi, huko Turkana. Kardinali John Njue, Rais
wa Baraza la Maaskofu Katoliki anasema, ukweli utawaweka huru na kwamba, jamii haiwezi
kuvumilia kuona usaliti ukifanywa na watu waliopewa dhamana ya kulinda usalama wa
raia na mali zao na kwamba, vitendo kama hivi si mara ya kwanza vinajirudia nchini
Kenya.
Kuna vitendo vya uhalifu vinavyopelekea watu kupoteza maisha na mali
zao, lakini mkondo wa sheria umekuwa unasuasua kuchukua hatua madhubuti, kiasi kwamba,
watu wanaanza kukosa imani na vyombo vya ulinzi na usalama.
Baraza la Maaskofu
linaitaka Serikali kuachana na maneno, na kuanza kutekeleza sera zake kwa vitendo,
ili kulinda haki, amani na ustawi wa wananchi wa Kenya. Katiba ambayo ni Sheria mama
iwalinde wanachi na Serikali ijitahidi kuwapatia huduma msingi kwani hadi sasa hata
baada ya miaka 50 ya Uhuru wa Kenya, kuna miji ambayo imesahaulika katika mchakato
wa maendeleo.
Baraza la Maaskofu katika tamko lao, lina sema, hakuna amani
ya kweli pasi na maendeleo endelevu ya watu. Maaskofu wanaiomba Serikali kushughulikia
kwa kina na mapana maeneo yote ya ardhi yenye umiliki wa utata hasa katika maeneo
ambayo yana utajiri mkubwa wa madini ili haki iweze kutendeka na hatimaye, kuondoa
kinzani za kijamii zinazokwamisha mchakato wa maendeleo endelevu.