2014-11-10 08:56:35

Askofu mkuu Richard Gallagher, Katibu mkuu mpya wa Mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Richard Gallagher kuwa Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Gallagher alizaliwa mjini Liverpool, Uingereza kunako tarehe 23 Januari 1954. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa kunako tarehe 31 Julai 1977.

Askofu mkuu Gallagher ana shahada ya uzamivu katika Sheria za Kanisa. Alianza kutoa huduma zake za kichungaji katika masuala ya kidiplomasia kunako tarehe Mosi, Mei 1984, kwa mara ya kwanza akatumwa kwenye Ubalozi wa Vatican nchini Tanzania. Katika masuala ya kidiplomasia amewahi kufanya utume wake kwenye Balozi za Vatican nchini Uruguay, Ufilippini na kama afisa kwenye Idara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican, kabla ya kuteuliwa kuwa ni Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Baraza la Umoja wa Nchi za Ulaya, utume alioufanya kuanzia tarehe 15 Julai 2000.

Tarehe 22 Januari 2004 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Burundi, mara baada ya mauaji ya kikatili ya Askofu mkuu Michael Aidan Courtney, yaliyotokea tarehe 29 Desemba 2003. Tarehe 19 Februari 2004, akawekwa wakfu katika Ibada iliyoongozwa na Kardinali Angelo Sodano, Katibu mkuu wa Vatican kwa wakati huo. Tarehe 19 Februari 2009, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Guatemala na tangu tarehe 11 Desemba 2012, akahamishiwa nchini Australia ili kuendelea na utume wake kama Balozi wa Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 8 Novemba 2014 akamteuwa kuwa ni Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano mjini Vatican kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Askofu mkuu Dominique Mamberti, ambaye ameteuliwa kuwa ni Mwenyekiti wa Mahakama kuu ya Kanisa mjini Vatican, anayechukua nafasi iliyoachwa wazi na Kardinali Raymond Leo Burke ambaye ameteuliwa kuwa mkuu wa Chama cha Kitume cha Malta.







All the contents on this site are copyrighted ©.