Waonesheni vijana kwamba ninyi ni Wamissionari wa matumaini na furaha!
Watawa wanaalikwa na Mama Kanisa kushiriki kikamilifu katika majiundo ya vijana wa
kizazi kipya kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji, kwani vijana wanapambana na
changamoto mbali mbali katika maisha yao, hasa kutokana na umaskini wa maisha ya kiroho
na kiutu; vijana wanapungukiwa na upendo pamoja na mahusiano thabiti ya kijamii.
Baba
Mtakatifu Francisko ameyasema hayo, Jumamosi tarehe 8 Novemba 2014, wakati alipokutana
na kuzungumza na wajumbe wa mkutano mkuu wa Shirika la Masista wa Bikira Maria msaada
wa daima. Baba Mtakatifu amewataka watawa hawa kuiga mfano wa Mtakatifu Yohane Bosco
na Mama Mazzarello, kwa kuwaonjesha vijana ujumbe unaofumbatwa katika upendo na huruma
ya Mungu kwa kila binadamu.
Baba Mtakatifu anawataka watawa hawa kutoka na
kuwaendelea watu wanaoishi pembezoni mwa Jamii kijiografia pamoja na kukosa mahitaji
yao msingi kama binadamu; kwa kutoa upendeleo wa pekee kwa maskini na wote wanaotengwa
kutokana na hali yao ya maisha.
Watawa wayasimike maisha yao katika mabadiliko,
toba na wongofu wa ndani unaojidhihirisha katika utekelezaji wa mikakati ya shughuli
za kichungaji, hili nyumba zao ziweze kuwa kweli ni mazingira ya Uinjilishaji kwa
kuwashirikisha vijana katika utume na maisha ya Kanisa. Wanapaswa kuwajibika kwa kuwasaidia
vijana katika hija ya maisha yao ya kiimani, ili hatimaye, vijana wenyewe waweze kushikamana
na Yesu na kuwa ni vyombo vya Uinjilishaji kwa vijana wenzao.
Watawa waendelee
kusikiliza sauti ya Roho Mtakatifu pamoja na kupokea neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu
pamoja na kutambua mahitaji msingi ya binadamu na kizazi ambacho kinakumbana na mabadiliko
makubwa. Waoneshe ushuhuda wa kinabii katika sekta ya elimu, ukarimu kwa vijana huku
wakikabiliana na changamoto za mwingiliano wa tamaduni, ili kupambanua njia muafaka
zinazoweza kutumiwa katika shughuli zao za kichungaji katika maisha ya vijana wanaoendelea
kuogelea katika ulimwengu wa mitandao na maendeleo ta teknolojia ya digitali.
Baba
Mtakatifu anasema, ili kuweza kufanikisha mikakati hii, kuna haja kwanza kabisa kumweka
Yesu Kristo kuwa ni kiini cha maisha yao, huku wakiongozwa na Neno la Mungu linalowaongoza
katika mikakati ya kimissionari pamoja na kudumu katika maisha ya sala; ushuhuda wa
maisha ya kidugu na kupokeana kama walivyo ili kukuza na kudumisha karama na zawadi
ambazo Mwenyezi Mungu amemkirimia kila mmoja wao, ili kuonesha kweli kwamba, wao ni
Wafuasi waYesu, jambo linalohitaji majiundo makini katika maisha ya kitawa yanayogusa
mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, pamoja na kuendelea kusoma alama za nyakati,
ili kumwilisha kikamilifu ujumbe wa Injili pamoja na kujisadaka kwa upendo.
Baba
Mtakatifu amegusia mambo msingi waliyojadili wakati wa maadhimisho ya mkutano mkuu
wa Shirika, kwa kuonesha furaha, majonzi na wasi wasi; pamoja na matarajio ya watu
wanaowahudumia. Wanapaswa kushikamana na vijana, watoto na wanawake kadiri ya hali
na mazingira yao, ili kuwaonesha kwamba, wao kweli ni wamissionari wa matumaini na
furaha, huku wakionesha tunu msingi za maisha ya watoto wa Mtakatifu Bosco; yaani
upendo kwa Mungu na vijana. Katika shida na mahangaiko kamwe wasikate tamaa, bali
waendelee kujielekeza zaidi na zaidi katika mchakato wa Uinjilishaji mpya kwenye sekta
ya elimu, katekesi na majiundo makini kwa vijana.
Baba Mtakatifu Francisko,
mwishoni, amekazia umuhimu wa maisha ya kijumuiya kama sehemu ya utekelezaji wa utume
wao ndani ya Kanisa, kwa kushuhudia kwamba, kweli wanajisadaka kwa ajili ya Mungu
na jirani.