2014-11-08 08:15:37

Radio Vatican inarusha matangazo yake kwa njia ya digitali!


Jukwaa la Kimataifa la Radio za Digitali, limehitimisha mkutano wake wa ishirini uliokuwa unafanyika mjini Roma, kwa kuwashirikisha wajumbe 120 kutoka katika vituo vya Radio za Umma na Binafsi, Barani Ulaya, Asia na Australia. Watengenezaji wa vifaa vya kielektroniki na magari walihudhuria pia. Hadi sasa, Uingereza na Uswiss ni nchi mbili ambazo zimefanikiwa kurusha matangazo ya Radio kwa njia ya mfumo wa digitali, nchi nyingine bado zinasuasua katika matumizi ya maendeleo ya teknolojia ya mawasiliano ya jamii.

Radio Vatican katika kipindi cha miaka 83 ya uhai wake imeendelea kusoma alama za nyakati kwa kufanya mabadiliko makubwa katika matumizi ya teknolojia ya mawasiliano, lengo ni kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu. Radio Vatican pamoja na mambo mengine anasema Padre Federico Lombardi, Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican na msemaji mkuu wa Vatican kwamba, inapania kutoa habari za Baba Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa na Ulimwengu.

Radio Vatican katika kipindi cha miaka 83 imejitahidi kurusha matangazo yake kwa njia ya Masafa Mafupi, SW, Masafa ya Kati, AM na Masafa Marefu, FM kwa kutumia mitambo ya analogia na kwa sasa Radio Vatican inarusha matangazo yake kwa kutumia mitambo ya digitali. Matangazo haya pia yanasikika kwa kutumia DRM "Digital Radio Mondiale", ingawa bado hakuna mafanikio makubwa kwani wasikilizaji wengi bado wanatumia mfumo wa zamani.

Ni matumaini ya Padre Lombardi kwamba, Radio mbali mbali za Majimbo na Mashirika zinazorusha matangazo ya Radio Vatican katika maeneo husika zitaweza kufanya mabadiliko katika teknolojia ili kuanza kutumia mfumo wa sasa wa digitali, ili kuwa uhakika wa ubora wa matangazo yanayotolewa. Radio Vatican inaendelea pia kuboresha kile kinachotangazwa na kwa nini kinatangazwa. Kipaumbele cha kwanza kinawekwa katika ujumbe na teknolojia inafuata, kwani inapaswa kuwa ni mhudumu wa ujumbe unaopania kumwendeleza mtu: kiroho na kimwili.








All the contents on this site are copyrighted ©.