2014-11-07 10:09:10

Wapambe nuksi!


Kila taifa na kabila hapa duniani lina utamaduni wake wa kusherekea mnuso wa arusi. Yasemwa kwamba huko uyahudini, mnuso wa arusi ulikuwa kabambe sana kiasi uliweza kudumu karibu wiki nzima. Ndoa ilikuwa inafungwa rasmi mwaka mmoja kabla, kishapo kila mwana arusi alirudi na kukaa nyumbani kwa wazazi wake kwa mwaka mmoja au zaidi kutegemeana na umri waliokuwa nao walipofunga ndoa.

Ilipofika wakati wa kuishi pamoja, bwana arusi alienda kumchukua bi arusi nyumbani kwa wazazi wake. Huko bi arusi alikuwa na wapambe yaani mabestigeli, watakaomsindikiza kwa bwana arusi huku wakiimba na kucheza.

Nyumbani kwa bwana arusi ndiko sherehe za ndoa zilikokuwa zinaendela kupamba moto kwa wiki mzima na zaidi. Kwa vile mambo hayo yalifanyika usiku, ilibidi wapambe hao wawe na taa za kujimulikia, na ingekuwa siku za leo ingewabidi wachukue tochi yenye betri. Yesu hakuwa mgeni na mazingira hayo ya mnuso kwani alikuwa anaalikwa mara nyingi kuhudhuria kama ilivyokuwa mnuso wa arusi ya Kana, ndiyo maana leo anatuletea mfano wa vituko vilivyowasibu wapambe hawa.

Lakini mnuso wa leo unatuingiza katika uwanja mwingine kabisa wa fasihi, siyo uwanja wa mifano kama tulivyozoea kusikia. Vitendo vilivyotumika viko katika wakati uliopita. Kwa hiyo, mfano huu unahusu upembuzi na utafiti au vyema zaidi kusema ni tathmini ya matendo yaliyoishafanyika. Katika upembuzi huo tunaletewa mshikeshike wa wasichana kumi: “Ufalme wa mbinguni utakapofanana na wanawali kumi waliotwaa taa zao, wakatoka kwenda kumlaki bwana arusi.”

Katika mnuso huu hatamkwi bi arusi. Yaonekana bi arusi yumo humohumo kwenye orodha hii ya wasichana kumi, namba inayomaanisha ukamilifu. Kwa vile jina hili Israeli (Wayahudi) katika nafsi ya kike (feminine), hiyo namba kumi ndiyo bi arusi mwenyewe. Kadhalika namba tano yamaanisha hao wapambe waliogawanyika kati ya wapumbafu na wenye busara. Hao wanawakilisha mgawanyiko wa Bi arusi huyo yaani Myahudi (Waisraeli). Yesu akautumia mfano huu akitaka kuuelekezea kwa taifa lake la wayahudi.

Kwa hiyo twaweza kuutafakari mfano huu katika mazingira ya Yesu jinsi alivyouelekeza yeye mwenyewe kwa Bi arusi wa kale, yaani taifa la Wayahudi; halafu katika mazingira ya Agano Jipya jinsi Mateo alivyouelekeza kwa Bi arusi ambayo ni jumuia ya kikristu ya wakati wake, au hata kuelekeza katika mazingira ya jumuia zetu siku za leo.

Tukianza na Taifa la Wayahudi, namba hii kumi ni idadi kamili ya watu walio pamoja wakimsubiri bwana arusi yaani Masiha, Yesu Kristu. Katika idadi hiyo kuna baadhi walimpokea na baadhi hawakumpokea. Kwa hiyo mfano huu ulimhusu Yesu mwenyewe na taifa lake la Wayahudi. Miaka hamsini baada ya Yesu, kukaibuka matatizo katika kanisa la wakristu wa Antiokia. Kisa kwamba wakristu hao walikuwa wamechoka, hawakuwa tena na motomoto na mhamasiko ule waliokuwa nao walipopokea dini ya Kikristu.

Wao walitegemea roho aliyetumwa na Yesu wakati anakufa, angekuwa ameenea tayari ulimwenguni kote. Kumbe hata baada ya kupita miaka hamsini hawakuona mabadiliko waliyoahidiwa kabla katika jumuia yao. Hivyo sasa taa ya imani na motomoto wa dini ukawa unafifia. Mwinjili Mateo ananukuu mfano huu ili kuwatia tafu hasa wale wapumbavu.

Ama kweli katika kila jumuia yoyote ya binadamu kuna makundi mawili. Kuna wapumbavu na wenye busara, kuna wema na wabaya, kuna magugu na ngano. Kadhalika kwenye mnuso wa arusi au popote penye sherehe utawakuta watu wanaotimuka kusherekea bila kujua mada ya mnuso, na wengine wanajua kinachoendelea.

Ndani ya kila mmoja wetu kuna bikira mwenye busara, anayelisha mwanga wa imani, (mafuta) lakini kuna pia huyu bikira mpumbavu anayetuacha wakati mwingine gizani. Sisi tuusome mfano huu na uwe mwanga kwetu, kusudi uweze kutusaidia kumgundua bikira mwenye busara atakayetuongoza na kutupatia vidokezo vya kumgundua bikira mpumbavu, iwe katika jumuiya au ndani ya nafsi yako mwenyewe.

Kuna pia kitendawili tega kimoja, kuwa Yesu hatuelezi mafuta hayo ni kitu gani. Kitendawili hicho kinabaki kuwa kazi kwetu kukitolea tafsiri. Kwa kweli mafuta hayo yanaweza kupata tafsiri nyingi sana. Kadiri yangu mimi mafuta hayo ni ule uwezo wa kupambanua mambo. Wale ”mabestigeli” wapumbavu walijisahau na shamrashamra za sikukuu wakijisemea: “Twendeni kwenye mnuso na huko tutajirusha hadi watukome”. Kwa hiyo walijimaindi zaidi wenyewe wakifikiria kujirusha na kujichana tu basi, pindi wale wenye busara, waliwa-maindi zaidi wana arusi, hasahasa kumshangilia Bwana arusi.

Aidha kuhusu kiasi cha mafuta nacho twaambiwa kwamba mabikira wenye busara walichukua taa na mafuta kiasi kidogo. Kumbe ilitosha kuwa na mafuta kidogo ya kushikilia utambi mradi koroboi iweze kuwaka daima. Mafuta hayo kidogo ni imani inayoleta mwanga na kumulika maisha ya dini ya mtu. Kwa hiyo vyombo hivyo vidogo, vingeweza kulinganishwana matendo madogomadogo tunayofanya ili kukuza imani, kama vile kusoma masomo Mtakatifu na kutafakari Neno la Mungu, kufanya semina na kozi mbalimbali za kiroho na kufanya fikara.

Misaada hiyo ni kama mafuta yanayolisha na kuongeza moto wa imani. Pasipo mafuta hayo, utambi unakauka na mwanga unafifia na ukipuliza upepo kidogo tu koroboi inazimika. Upepo huo unaweza kuwa vurugu za maisha, programu za kwenye luninga, simu za kisasa zenye kila kitu ndani, au hata katika kupiga michapo na wapumbavu, imani yetu inapungua na tunaanza kufikiri na kuongea kama wapumbavu wengine wa ulimwengu huu.

Taa hizi hata kama ndogo na mafuta kidogo, lakini zatosha kutuangazia tunapomsubiri bwana arusi usiku pindi sote tunalala. “Hata bwana arusi alipokawia, wote wakasinzia wakalala usingizi.” Hata sisi katika udhaifu wetu wa kibinadamu kuna wakati tunalegea na kulala usingizi. Inafaa kuongeza mafuta kidogo katika taa zetu na siyo kujisahau hadi taa inazimika kabisa.

“Lakini usiku wa manane pakawa na kelele, Haya bwana arusi, tokeni mwende kumlaki”. Usiku wa manane haina maana ya mwisho wa dunia au kifo, bali yamaanisha kila wakati Mungu anapofika katika maisha yetu. “Kwa maana majira mambo yote yalipokuwa kimya, na usiku ulikuwa katikati ya mwendo wake mwepesi, Neno lako Mwenyezi alishuka mbinguni kutoka kiti chako cha kifalme shujaa aliye hodari katika nchi iliyopasishwa hukumu, wenye upanga mkali, ndio amri yako isiyopindika...” (18:14-15).

Huo ni wakati wa kuondoka siyo wa kujiandaa. Kwa hiyo yabidi daima kuwa tayari kwa sababu hamjui siku wala saa atakayokuja mwana wa Adamu. Wapumbavu hawafanyi kitu badala yake wanaomba msaada kwa wenzao wenye busara: “Tupeni mafuta yenu kidogo; maana taa zetu zinazimika.”

Wanaishia kupata jibu kali usilolitegemea toka kwa wasichana hawa wenye busara: “Hayatatutosha sisi na ninyi; afadhali shikeni njia mwende kwa wauzao, mkajinunulie.” Kadhalika wanaporudi baadaye wanapata jibu la kukatisha tamaa toka Bwana arusi: “Ondokeni siwajui”.

Fundisho na maana halisi ya mfano huu siyo ukali wa jibu, bali tunafundishwa suala la kuwajibika na uhuru wa mtu binafasi. Kwamba kila mtu yabidi awajibike mwenyewe. Mtu huwezi ukajichana badala ya mtu mwingine, kadhalika huwezi ukapenda badala ya mwingine; huwezi ukawa mwema na mwaminifu badala yangu. Kama mimi mwenyewe siwajibiki juu yangu basi hakuna tena mtu mwingine atakayewajibika badala yangu.

Kadhalika Injili haihukumu hali ya kujisahau kwa siku moja (jioni moja) anakoweza kuwa nako mtu bali unaonekana kukosa busara pale unapoyapitisha maisha bila kukereketwa na imani uliyopokea. Toka ubatizwe mtu humfikirii kabisa Bwana arusi au walau kutunza mwanga wa ndani ulio katika akili, katika macho, katika maneno, katika moyo au pengine hata kutomwangaza mwingine na kumfumbua macho.

Kwa hiyo mfano huu unatuhimiza na kututisha, lakini pia unatutuliza. Maana yake hata kama ni usiku na mafuta ni kidogo lakini tuna uhakika Bwana anakuja. Kukawia kwake kuja kunatuchosha hadi wakati mwingine tunaweza kulala. Lakini kumbe katika giza la usiku wa manane, sauti inatuamsha, hapo tunajua kwamba Mungu anakuja hata kama anakawia huyo ndiye anayenituliza.

Halafu tena jinsi Bwana arusi anavyojibu ovyo na ukali yamaanisha, jinsi hukumu inayotolewa ilivyo mbaya. Kwa sababu pale anapoingia Bwana arusi kwenye mnuso ndipo inakuja hukumu ya maisha. Hapo ndipo atakapojulikana ni mtu aina gani atakayekaribishwa katika mnuso wa arusi. Kwa hiyo yabidi kuwa tayari sasa kumpokea Bwana arusi anayejionesha daima katika jumuia. Tunakuwa na furaha pale tunapompokea Bwana arusi na kujiacha tuongozwe naye kwenda kwenye jumba la mnuso arusi yaani katika ufalme wake.

Nje ya ufalme wa Mungu yaweza kuwa ni maburudisho ya kawaida na shamrashamra za nje nje, lakini hakuna furaha ya kweli, kwani baada ya shamrashamra hizo kunafuata kukata tamaa, kwani hakuna mahusiano na Bwana arusi, hakuna amani na wapambe wengine wenye busara, na mbaya zaidi hakuna furaha ya ndani. Mfano huu unataka pia kutuambia kuwa mwisho wa maisha haya kutakuwa pia kuingia kwenye jumba lililojaa nderemo za mnuso wa arusi isiyo na mwisho.

Lakini yabidi kuangalia jinsi maisha yalivyo, yaani ni nani anayeongoza maamuzi ya maisha yetu, Je, ni bikira mwenye busara, yaani roho ya Kristu aliye ndani ya kila mmoja wetu ya kupenda kama yeye alivyopenda au tunaongozwa na bikira mpumbavu anayetupeleka kwenye ubinafsi. Katika maana hii huwezi ukabadilisha mafuta.

Lugha ya mpumbavu na mwenye busara ilitumika pia katika ujenzi wa nyumba. Mtu mwenye busara anajenga nyumba juu ya mwamba, na mpumbavu anajenga nyumba juu ya mchanga. Tunaaswa kujiuliza Je, tunajiachia kuongozwa na bikira mwenye busara anayetupeleka kuishi kama Kristo au na bikira mpumbavu anayetutenga mbali na Kristo.

Padre. Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.