Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema kwamba, maadhimisho
ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, ambao muhtasari wake umewekwa kwenye
Hati ya Mababa wa Sinodi inayojulikana kama "Relatio Synodi" itakayotumiwa wakati
wa maadhimisho ya Sinodi ya Kawaida ya Maaskofu kuanzia tarehe 4 hadi tarehe 25 Oktoba
2015 inaonesha wito, utume na dhamana ya Mama Kanisa katika mchakato wa kutangaza
Injili ya Familia kwa Watu wa Mataifa.
Hii ni changamoto kwa Makanisa mahalia
kuendelea kukazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia mintarafu sheria, kanuni
na Mapokeo ya Mama Kanisa. Hati hii inaonesha changamoto mintarafu Mafundisho ya Mababa
wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na Mapokeo ya Kanisa kadiri yalivyofafanuliwa
na viongozi wa Kanisa kwa nyakati mbali mbali, ili kukuza na kudumisha tunu msingi
za maisha ya ndoa na familia, kama nguzo thabiti za ujenzi wa Familia kama Kanisa
dogo la nyumbani.
Familia inapaswa kuwa ni shule ya utu na heshima ya binadamu;
kitalu cha Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili
na kwamba, Familia ni Kanisa dogo, linalotoka kuwaendelea Watu wa Mataifa ili kushuhudia
kwa njia ya maneno na mifano adili ya maisha, Injili ya Familia. Ili kufikia lengo
hili, Familia hazina budi kutekeleza dhama yake msingi ya malezi na majiundo kwa watoto
na vijana wa kizazi kipya, kwa kuwashirikisha mang'amuzi ya maisha yanayojikita katika
uzoefu wa imani na tunu msingi za maisha ya ndoa na familia. Wanafamilia wanahamasishwa
kuwa kweli ni shule ya upendo na huruma, kwa kusaidiana, kufarijiana na kutaabikiana
katika safari ya maisha ya kila siku.
Mababa wa Sinodi katika majadiliano yao
wamekiri kwamba, Familia ni mahali ambapo wanafamilia wanajifunza kujenga na kudumisha
mahusiano ya kijamii, kumbe Familia ni shule ya mahusiano ya kijamii, ni shule maisha
na utume wa Kanisa; ni madhabahu ya zawadi ya maisha, mahali ambapo maisha yanalindwa
na kuendelezwa katika hatua mbali mbali. Hapa familia inakumbushwa kwamba ni sehemu
muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa, dhamana inayotekelezeka kwa njia ya
majiundo makini ya watoto katika masuala ya kiimani, kiutu na kitamaduni.
Mababa
wa Sinodi wamewataka wanafamilia kuhakikisha kwamba, wanajenga na kudumisha mahusiano
kati ya vijana wa kizazi kipya na wazee ambao ni "Maktaba rejea" ya tunu msingi za
maisha ndani ya jamii; bila kusahau kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya ndoa, Bwana
na Bibi wanaunga na kuwa ni mwili mmoja, tukio ambalo pia linaunganisha familia mbili
tofauti na hivyo kuanza kutembea kwa pamoja na katika mshikamano wa upendo.
Kuna
hatua kubwa ambayo imefikiwa na Jumuiya ya Kimataifa katika kukuza na kudumisha haki
msingi za binadamu, uhuru na utu wa binadamu. Lakini kwa upande mwingine ni mambo
ambayo yanapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa, ili haki binafsi zisiharibu tunu msingi
za maisha ya ndoa na familia kwa kutaka kuhalalisha hata mambo yale ambayo kimsingi
ni dalili za kumong'onyoka kwa utu na heshima ya binadamu; upweke hasi na mahusiano
tenge kati ya watu.
Mababa wa Sinodi wanabainisha kwamba, licha ya mapungufu
haya ya kibinadamu, Kanisa kwa upande wake linapenda kusimama kidete kulinda na kutetea
tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa ajili ya mafao na ustawi wa familia
ya binadamu pamoja na kuziwezesha familia kutekeleza dhamana ya kutoa majiundo makini
kwa watoto wao.
Mama Kanisa anaangalia haki na huruma kama mambo ambayo yanaweza
kusaidia kukuza maisha ya ndoa na familia. Mafao ya Familia hayana budi kumwilishwa
katika uhalisia wa maisha, vinginevyo yataendelea kuelea katika ombwe, bila kuwa na
mafao kwa familia zenyewe. Kardinali Lorenzo Baldisseri anasema, Kanisa katika maadhimisho
ya awamu ya kwanza ya Sinodi kwa ajili ya familia limeanza safari ndefu ya kutangaza
Injili ya Familia, safari inayohitaji mchango wa hali na mali kutoka kwa kila familia!