Mambo ya Kale ni ushuhuda wa maisha na utume wa Kanisa!
Roma ni mji ambao unahifadhi kumbu kumbu nyingi za kihistoria, mambo ambayo yana utajiri
mkubwa katika historia, maisha na utume wa Kanisa. Ni mahali ambapo kuna chimbuko
la imani na tamaduni ambazo zimesaidia kuleta mchakato wa mabadiliko katika maisha
ya mwanadamu: kiroho, kimwili na kitamaduni.
Ni mji unaonesha shuhudi za imani
zilizotolewa na miamba wakuu wa Kanisa kama vile Mtakatifu Petro na Paulo, ambao kwa
njia ya ushuhuda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, leo Kanisa limeenea sehemu
mbali mbali za dunia. Kanisa limeendelea kuwaenzi wafiadini, waliojisadaka maisha
yao kwa kutunza kwa heshima kubwa makubiri yanayopatikana mjini Roma. Hawa ni vielelezo
vya imani ya Kanisa kuhusu mateso, kifo na ufufuko wa Yesu, unaowakarimia waamini
maisha mapya yanayofumbata uzima wa milele.
Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa
na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, tarehe 6 Novemba 2014,
wakati wa kuzindua Mwaka wa Masomo wa Taasisi ya Kipapa ya Mambo ya Kale. Watu wanahimizwa
kutunza utajiri huu kwa ajili ya mafao ya kizazi kijacho na kwamba, Papa Pio wa kumi
na moja aliona umuhimu wa utunzaji za kumbu kumbu za kale ndiyo maana akaanzisha taasisi
ya kipapa kwa ajili ya mambo ya kale, ambayo yana maana sana katika maisha na utume
wa Kanisa.
Hii ni taasisi ambayo inatoa masomo kwa vijana kutoka sehemu mbali
mbali za dunia, wanaofika hapo ili kujifunza kwa kina na mapana jinsi ya mambo ya
kale; kwa kuona kwa macho yao wenyewe pamoja na kushiriki katika makongamano mbali
mbali ya kitaifa na kimataifa, mambo msingi kama sehemu ya mchakato endelevu wa kitaaluma.
Kardinali Pietro Parolin anawatakia wote heri na fanaka katika masomo na maisha yao
ya kila siku.