2014-11-07 09:06:20

Komesheni mauaji ya watu wasiokuwa na hatia huko Mashariki ya Kati!


Askofu mkuu Bernadito Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, hivi karibuni akishiriki katika mkutano wa 69 wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa ametumia fursa hii kutoa salam zake za rambi rambi kwa familia za wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa waliouwawa kikatili wakati wakitoa msaada kwa wakimbizi wa Palestina.

Hadi sasa inaonekana kwamba, mchakato wa amani katika Ukanda wa Ghaza bado unechechemea na matokeo yake watu wanaendelea kupoteza maisha pamoja na uharibifu wa miundo mbinu. Vatican inapenda kuiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inakomesha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia; kwa kudhibiti biashara haramu ya silaha huko Mashariki ya Kati ili fedha hiyo iweze kutumika kuchochea huduma na maendeleo ya watu.

Vatican inapenda kuonesha mshikamano wake na Wakristo wanalazimika kuyakimbia makazi yao huko Mashariki ya Kati kutokana na nyanyaso na dhulumu za kidini na kwamba, Kanisa Katoliki kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, litaendelea kutoa huduma ya elimu, afya na maendeleo kwa wananchi wengi wanaoishi vijijini bila ubaguzi, mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kuonesha mshikamano wa upendo na udugu kwa wananchi wanaoishi huko Mashariki ya Kati.

Askofu mkuu Auza anasema kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inashiriki katika mchakato wa upatikanaji wa amani huko Mashariki, lakini Israeli na Palestina wanapaswa kutambua kwamba, wao ndio wadau wakuu, wanaopaswa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kujenga na kudumisha uhuru wa kidini ili kweli amani iweze kutawala katika mioyo ya watu.







All the contents on this site are copyrighted ©.