2014-11-07 14:53:43

Jengeni shuhuda zenye mvuto na mashiko katika maisha ya watu!


Maisha ya Kitawa yanaliwezesha Kanisa kuwa na mvuto na mashiko kutokana na shuhuda zinazotolewa na Watawa katika huduma mbali mbali katika maisha yanayojikita katika sadaka inayojionesha kwa namna ya pekee kwa kumfuasa Kristo, huku wakiwa wamejitwika Misalaba yao, mwaliko na changamoto kwa watawa kutoa ushuhuda wa kinabii unaosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili, Utakatifu pamoja na kusoma alama zanyakati.

Hayo yamesemwa na Baba Mtakatifu Francisko Ijumaa, tarehe 7 Novemba 2014, wakati alipokutana na kuzungumza na Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume nchini Italia waliohitimisha mkutano wao wa mwaka. Baba Mtakatifu anawashukuru kwa kufanya tafakari ya kina kuhusu Waraka wake wa kichungaji Injili ya Furaha, yaani "Evangelii gaudium" ili kutangaza na kueneza Ufalme wa Mungu, unaohitaji toba na wongofu wa ndani; sala, tafakari na Ibada ya kuabu; tayari kujisadaka kwa ajili ya kuwaendea wale wanaoishi pembezoni mwa Jamii.

Baba Mtakatifu anasema, Watawa wanapaswa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo endelevu wa Yesu katika maisha, huku wakiendelea kumwilisha karama zao katika maisha na utume wao ndani ya Kanisa, ili kwa ujasiri na ushuhuda wa maisha ili karama hizi ziweze kuzaa kwa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha, tamaduni na historia kama Wamissionari wengi kutoka katika Mashirika haya walivyofundisha.

Baba Mtakatifu anasema, maisha ya kitawa hayana budi kujikita katika udugu, ili kuondokana na utamaduni mamboleo unaoendekeza haki za mtu binafsi; utamaduni unaoharibu msingi wa maisha ya kifamilia, kumbe ni wajibu wa Mashirika ya kitawa kuonesha shuhuda za udugu kwa kuishi pamoja hata katika utofauti wao, kwani hili ndilo fumbo la maisha ya kijumuiya, hakuna mtawa anayechagua mtu wa kuishi naye.

Pale watawa wanapoteleza na kuanguka dhambini, wawe na ujasiri wa kusimama tena ili kufanya toba na hatimaye, kujipatia neema inayopatikana kutoka kwenye kitubio, mambo msingi katika maisha Kijumuiya kwa ajili ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Jumuiya za kitawa zinajengeka katika msingi wa Ubaba wa Mwenyezi Mungu na Umama wa Kanisa na Bikira Maria; mahusiano ambayo daima yanajengwa na kudumishwa kwa njia ya: Sala, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu pamoja na Rozari Takatifu.

Kwa njia hii watawa wanaweza kuwa na ujasiri wa kuendelea kukaa pamoja na Yesu Kristo, ili kudumisha mahusiano na Mwenyezi Mungu, Bikira Maria na Kanisa katika ujumla wake. Kwa njia ya mahusiano haya, watawa wanaweza kufanikiwa kujenga na kushuhudia udugu wa kweli wenye mvuto na mashiko. Baba Mtakatifu anawaalika watawa kuendelea mbele katika hija hii ya maisha na kwamba, kwa njia yao anapenda kubariki Jumuiya zao za kitawa lakini zaidi kwa wazee na wagonjwa.







All the contents on this site are copyrighted ©.