2014-11-07 07:15:59

Changamoto katika mapambano dhidi ya uhalifu wa kimataifa!


Jumuiya ya Kimataifa inaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 100 tangu Jeshi la Polisi Kimataifa, Interpol lilipoanzishwa, mwaliko kwa vikosi vya ulinzi na usalama kushirikiana kwa karibu zaidi katika kupambana na changamoto za ulinzi na usalama kwa nyakati hizi.

Uwepo wa Interpol umesaidia kuimarisha ulinzi na usalama kwa familia ya binadamu na kwamba, Vatican itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa ili kuenzi juhudi, kwa kukazia utawala wa sheria, haki, amani, utu na heshima ya binadamu.

Huu ni mchango uliotolewa na Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican wakati wa mkutano wa themanini na tatu wa Interpol, ulioanza hapo tarehe 3 hadi tarehe 7 Novemba 2014, huko Monaco. Anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake, anaendelea kuwahimiza watu wa mataifa kujenga na kudumisha utamaduni wa kukutana unaopania kuimarisha mahusiano ya kijamii, utu, heshima ya binadamu na mshikamano kati ya watu.

Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, uhalifu wa kimataifa umeongezeka maradufu, kutokana na: mwingiliano wa watu, wepesi wa kusafrisha fedha na bidhaa na matokeo yake ni kama vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati. Uhalifu wa kimataifa unatumia silaha kali na zinazosababisha uhalibifu mkubwa. Jumuiya ya Kimataifa inakabiliana pia na biashara haramu ya binadamu inayojionesha katika sura mbali mbali mambo ambayo kamwe hayawezi kukubalika.

Askofu mkuu Mamberti anasema, Vatican itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika malezi ya dhamiri nyofu, kwa kukazia haki msingi za binadamu, utu na heshima yake; uhuru na wajibu wa Serikali husika katika kudumisha utawala wa sheria. Pengo kubwa la maendeleo kati ya watu ni chanzo kikubwa kinachosababisha mipasuko ya kijamii na matokeo yake ni kinzani na vita; mambo ambayo pia yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na mtikisiko wa uchumi kimataifa. Maendeleo ya sayansi ya mawasiliano ya jamii yamekuwa pia ni tishio kwa amani na usalama wa Jumuiya ya Kimataifa.

Askofu mkuu Mamberti anasema kuna haja ya kukuza na kudumisha utawala wa sheria, mahusiano bora ya kijamii kwa kuzingatia tamko la Umoja wa Mataifa kuhusu haki msingi za binadamu; utu na heshima ya binadamu pamoja na kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi. Ikumbukwe kwamba, binadamu ana haki na wajibu anaopaswa kutekeleza hata pale anapopatikana na hatia ya kuvunja sheria. Adhabu ilenge kuleta maboresho katika maisha ya mhusika ili anapohitimisha adhabu yake aweze kurejea tena katika Jamii na kuendelea na maisha kama kawaida.

Askofu mkuu Dominique Mamberti anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kutumia rasilimali watu na fedha kwa ajili ya maendeleo ya watu: kimaadili, kitamaduni na kiuchumi, kwani maendeleo na mshikamano wa kimataifa ni jina jipya la amani ya kudumu. Serikali pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vikifanikiwa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika mazingira kama haya, hapo Jamii inaweza kupambana fika na uhalifu.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuendelea kuwekeza katika mapambano dhidi ya: uhalifu na ufadhili dhidi ya vitendo vya kigaidi; ugaidi wa kibailojia, utakatishaji wa fedha haramu, biashara haramu ya silaha ambayo ni chanzo kikuu cha majanga ya kitaifa na kimataifa pamoja na biashara haramu ya binadamu, inayodhalilisha utu na heshima ya binadamu.

Vatican katika siku za hivi karibuni imeweka sheria na mikakati ya kupambana kikamilifu na vitendo hivi na kwamba, itaendelea kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa, ili kufanikisha malengo haya!

Imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.