Ujumbe wa amani na matumaini kwa wananchi wa Burkina Faso!
Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso katika mkutano wake wa siku mbili uliohitimishwa
hivi karibuni, limetoa ujumbe wa amani na matumaini kwa wananchi wa Burkina Faso,
kwa kuwataka kuwa kweli ni wajenzi na vyombo vya haki, amani na upatanisho.
Kanisa
linatambua dhamana na wajibu wake wa kuwa ni vyombo vya huduma ya haki, amani na upatanisho
na kwamba, kama Kanisa, waliwahi kuonya kwamba, vijana wengi nchini Burkina Faso walikuwa
wamekata tamaa na kuchangayikiwa na kwamba, hali hii ilipaswa kurekebishwa mapema
kabla ya madhara makubwa hayajatokea! Lakini Waswahili wanasema, usipoziba ufa utajenga
ukuta!
Maaskofu wanakumbusha kwamba, Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI alipotembelea
nchini Benin kunako mwaka 2011 ili kuzindua matunda ya Awamu ya Pili ya Sinodi maalum
ya Afrika, akizungumza na viongozi wa kisiasa na wachumi kutoka Barani Afrika, aliwataka
kutowapokonya watu wao matumaini ya kesho iliyo bora zaidi, kwa kuwawekea giza, bali
wahakikishe kwamba,wanawajibika kimaadili na daima wakijitahidi kutafuta hekima ya
Kimungu, ili waweze kufahamu mapenzi ya Mungu kwa ajili ya watu wao, ili hatimaye,
waweze kuwa ni vyombo vya matumaini.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi
na sita, aliwaambia viongozi wa Bara la Afrika kwamba, si rahisi kuhimili kishindo
cha vishawishi na majaribu katika ulimwengu mamboleo kwa kutambua kwamba, uongozi
ni huduma kutokana na uchu wa mali na madaraka mambo ambayo yanawatumbukiza viongozi
wengi kushindwa kusimama kidete kulinda na kutetea mafao ya wengi na matokeo yake
kuendekeza: ubinafsi, ukabila na udini. Ni Mungu mwenyewe anayeweza kuwakirimia waja
wake nia njema.
Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linapenda kuungana
na wale wote waliopoteza ndugu zao wakati wa machafuko na maandamano yaliyopelekea
Serikali iliyokuwa madarakani "kubwaga manyanga". Wanapongeza juhudi za uzalendo zinazooneshwa
na wananchi kwa kusema kwamba, sasa ni wakati wa kufutilia mbali maovu kutoka katika
undani wa mioyo yao na katika miundo mbinu ya kijamii; kulinda maisha na mali ya watu.
Maaskofu wanawaalika waamini na wananchi wa Burkina Faso katika ujumla wao,
kuanza kujikita katika mchakato wa uponyaji wa ndani kwa kuwashughulikia wale walioguswa
kwa namna ya pekee na machafuko ya kisiasa nchini humo, ili kudumisha ulinzi na usalama
wa watu na mali zao; changamoto ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu.
Maaskofu
katika barua yao ya kichungaji wanawataka wananchi wa Burkina Faso kuzingatia na kuheshimu
utawala wa sheria na vyombo vya ulinzi na usalama; waandishi wa habari watekeleze
wajibu wao kwa kuzingatia kanuni maadili, uzalendo na mustakabali wa taifa lao. Viongozi
mbali mbali nchini humo waunganishe nguvu zao ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano
wa kitaifa, kwa ajili ya Bukrina Faso mpya.
Imehaririwa na Padre Richard
A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.