Mwongozo kwa Makardinali na Maaskofu kung'atuka kutoka madarakani
Baba Mtakatifu Francisko katika mazungumzo yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu
mkuu wa Vatican hapo tarehe 3 Novemba 2014, amemruhusu achapishe kanuni zitakazotumika
kwa ajili ya Maaskofu wa Jimbo na viongozi wote wa Kanisa wanaoteuliwa na Khalifa
wa Mtakatifu Petro kushika nyadhifa mbali mbali ndani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu
anawaalika kwa namna ya pekee, wahusika kuhakikisha kwamba, wanafuata sheria na kanuni
zilizopo kwa kutambua kwamba, Uaskofu ni huduma na wala si cheo. Maaskofu wanapaswa
kuandika barua ya kung'atuka kutoka madarakani wanapotimiza umri wa miaka 75. Ombi
hili linapokubaliwa na Baba Mtakatifu, madaraka yote aliyo nayo mhusika hata katika
ngazi ya kitaifa yanasitishwa mara moja.
Katika mwelekeo huu, Familia ya Mungu
inachangamotishwa kwa namna ya pekee kabisa kuonesha moyo wa upendo na mshikamano
kwa aliyekuwa kiongozi wa maisha yao ya kiroho, kwa kuzingatia kanuni ya haki na upendo.
Katika mazingira maalum, viongozi wanaohusika wanaweza kumwomba Askofu kuandika barua
ya kung'atuka kutoka madarakani, baada ya kumsikiliza kwa umakini mkubwa na katika
majadiliano ya kidugu.
Makardinali na wakuu wa Taasisi za Kipapa pamoja na
Makardinali wanaotekeleza dhamana yao kwa kuteuliwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro;
watatakiwa wafikishapo umari wa miaka 75 kuwasilisha ombi la kung'atuka kutoka madarakani
kwa Baba Mtakatifu, atakayetolea maamuzi kwa wakati wake. Wakuu wa Mabaraza na Taasis
za Kipapa, Makatibu wakuu na Maaskofu wanaotekeleza dhamana yao kwa uteuzi wa Baba
Mtakatifu, dhamana yao ufika ukomo wanapotimiza umri wa miaka 75; wajumbe wanapotimiza
umri wa miaka 80 dhamana na huduma yao inasitishwa mara moja.