Mkimbilieni Mwenyezi Mungu ili muonje huruma na upendo wake katika Sakramenti ya Upatanisho!
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha
kilichoko mjini Vatican, Alhamisi tarehe 6 Novemba 2014 amewataka Wakristo kuonesha
moyo wa toba kwa kukimbilia Sakramenti ya Upatanisho, ili kuonja huruma na upendo
wa Mungu unaotolewa na Mama Kanisa kwa njia ya Wahudumu wa Injili, ili waweze kujipatia
wokovu na uzima wa milele.
Baba Mtakatifu anasema inasikitisha kumwona Padre
akiwa amefungua mlango wa Kanisa na kuendelea kusubiri waamini kuja kuungama na hakuna
anayejitokeza, lakini mbaya zaidi kwa waamini ambao hawaoni tena sababu ya kutubu
na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Viongozi wa Kanisa hawana budi kuhakikisha kwamba,
wanajitahidi kadiri ya uwezo wao kuwaganga wale waliovunjika moyo bila ya kukata tamaa
kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kila mtu aweze kuokoka na kupata uzima
wa milele.
Yesu Kristo aliyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu
kutoka katika lindi la dhambi na mauti, changamoto na mwaliko kwa viongozi wa Kanisa
kutoogopa kuwaendelea na kuwahudumia wadhambi, ili waonje huruma na upendo wa Mungu
katika maisha yao. Kanisa linawahitaji viongozi wema na watakatifu, linataka kuwaona
Wakristo wema na watakatifu pia, ili kwa pamoja waweze kumwomba na kumwabudu Mwenyezi
Mungu, kwa kuwatangazia wengine Habari Njema ya Wokovu.