Mambo ya kuzingatia katika kupambana na baa la umaskini duniani!
Jumuiya ya Kimataifa katika kipindi cha miaka kumi, yaani kuanzia mwaka 2008 hadi
mwaka 2017 ilijiwekea mkakati wa kupambana na baa la umaskini duniani, utekelezaji
wa Malengo ya Maendeleo ya Millenia sanjari na kuweka sera bora za maendeleo endelevu.
Hii ni changamoto endelevu kwa Jumuiya ya Kimataifa kutokana na ukweli kwamba, bado
baa la umaskini linaendelea kuyaandama mallioni ya watu duniani.
Sera na mikakati
ya mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato zizingatie kwa namna ya pekee hali
halisi, uzoefu na mang’amuzi ya watu kuliko mtindo wa sasa wa kutoa sera ambazo zimekwisha
andaliwa kwenye maabara ambazo hazitekelezeki na matokeo yake watu wanaendelea kuogelea
katika dimbwi la umaskini. Sera makini na siasa bora ni nyenzo msingi katika mapambano
dhidi ya baa la umaskini, kwa kuwahusisha watu wenyewe pamoja na kujenga mshikamano
wa dhati ndani ya Jamii.
Ni changamoto iliyotolewa hivi karibuni na Askofu
mkuu Bernaditto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati
akichangia hoja kwenye Baraza kuu la Umoja wa Mataifa, lililokuwa linajadili mikakati
ya kupambana na baa la umaskini duniani. Maendeleo ya kweli yanajikita katika sera
makini zinazowahusisha wadau katika medani mbali mbali za maisha, sanjari na kutoa
kipaumbele cha kwanza kwa binadamu kama mlengwa mkuu wa maendeleo.
Askofu mkuu
Auza anasema, sera nyingi zilizoibuliwa na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi
ya baa la umaskini, bado hazijaonesha mafanikio makubwa, kwani watu wanaendelea kutumbukia
katika umaskini wa hali na kipato, mambo yanayo nyanyasa utu na heshima ya binadamu.
Wanawake wanapaswa kupewa fursa na haki sawa katika mchakato wa utekelezaji wa sera
na mikakati ya maendeleo kwani katika sehemu nyingi duniani wanawake “ ni majembe”
ya mandeleo.
Na takwimu zinaonesha kwamba, waathirika wakubwa wa balaa la
umaskini ni wanawake na watoto; hali ambayo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na ubaguzi
katika utoaji wa huduma msingi za kijamii kama vile elimu, afya, utamaduni, kisiasa
na mwelekeo wa maisha ya kiroho.
Ikumbukwe kwamba, mchakato wa kupambana na
baa la umaskini haulengi kuwaongezea watu fedha mifukoni, bali ni kuhakikisha kwamba,
mtu mzima anakombolewa kutoka katika umaskini na hivyo kumwezesha kupata ustawi na
maendeleo ya kweli: kiroho na kimwili; changamoto kwa kila mtu kuchangia ili kweli
Jumuiya ya Kimataifa iweze kufikia lengo hili linalopania kuwafaidia wengi kwa kuongozwa
na kanuni ya mshikamano.