2014-11-05 07:23:26

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka A wa Kanisa


Mpendwa msikilizaji tunakuleteeni habari njema ya furaha, tukikualika ushiriki nasi siku njema inayopambazuka kwa Neno la upendo, Dominika ya 32 ya mwaka A wa Kanisa. Ujumbe ni huu “kaeni tayari kumpokea Bwana arusi ndiye Masiha mkombozi, itafuteni hekima ya Mungu kwa njia ya Neno lake wakati wote ili siku ijapo ikukute uko tayari”. RealAudioMP3

Katika somo la kwanza mwandishi anaweka mbele yetu hekima kama uwezo wa kuishi vizuri, kuwa na subira katika kutoa maamuzi, kuchagua maneno ya kusema, upole, unyenyekevu na zaidi kuwa na kiasi katika kutenda. Kwa maelezo haya twaona kuwa hekima ni jambo jema mno ambalo linajenga jumuiya na lakuza utu wa mtu. Je, jambo hili jema latoka wapi? Kadiri ya wanamaandiko hekima yatoka juu, yatoka kwa Mungu.

Kadiri ya somo la kwanza hekima hii imepambwa kwa uzuri, inang’aa na huonekana upesi kwa wanaoitafuta. Kadiri ya uzuri huu tunaona ni upendo wa Mungu ungaao bila kufifia, ni hekima ya Mungu itokayo juu, ni Neno lake. Mpendwa mwana wa Mungu, unaalikwa leo na Neno la Mungu kuchuchumalia yaliyo ya juu na kwa namna hiyo kukaa tayari katika hekima hiyo ili bwana arusi ajapo akukute uko tayari.

Katika somo la pili, Mtume Paulo anatuambia juu ya mambo ya mwisho akisema, ufufuko ndiyo shime yetu kwa maana Kristu alikufa na kufufuka na hivi kwa yeyote katika Kristu hakuna mauti endelevu bali mauti mpito kuelekea utukufu. Anasema, msiogope enyi Watesalonike kwa maana parapanda ya Mungu ikilia waliolala watafufuliwa kwanza na kisha nasi tutanyakuliwa. Mtume Paulo anatoa fundisho hili kwa sababu Watesalonike wana mashaka juu ya ndugu zao waliokwishalala katika mauti kama watafufuliwa.

Na mashaka haya yameingia katika nyoyo zao kwa sababu walimu katika Israeli walifundisha ujio wa haraka wa Bwana. Mashaka hayakuishia tu katika waliolala hata wengine waliamua kuacha kufanya kazi wakisubiri ujio wa pili ulio wa haraka!

Ndiyo kusema, Mtume Paulo anawambia jambo msingi ni ubatizo ambao kwao mkristu anaingia katika uzima wa milele, kumbe kifo si mwisho bali mpito kuelekea maisha mapya. Pili anawafundisha kuwa Kristu amefufuka na hivi kifo hakina nguvu juu ya mwanadamu. Kwa namna hiyo wale wote waliounganika naye kwa ubatizo na hivi wamelala katika Kristu watafufuliwa na kuingia katika utukufu wake wa milele. Jambo la Bwana atakuja lini linapaswa kueleweka katika kukaa tayari daima na hii ndiyo imani yetu.

Mpendwa msikilizaji, Injili ya Dominika ya 32 yatufundisha kuwa tayari daima katika maisha yetu na hivi ndiyo kuwa na hekima ya kimungu, ndiyo kuitafuta hekima ambayo yatujia kila siku kwa njia ya neno lake. Mfano wa wanawali kumi waliokwenda kumlaki Bwana, watano wakiwa na taa zenye mafuta ambao ndio kielelezo cha hekima na busara na watano wasiokuwa na mafuta bali taa tu, yaani walio wapumbavu watuonya vema kuwa makini, tunapoendesha maisha ya kikristu.

Kuwa na taa zenye mafuta maana yake ni kushika vema mausia ya Neno aliyefanyika mwili na akakaa kwetu. Ni kuingia kwenye maisha ya jumuiya ya Kikristu. Ndiyo kusema kushika amri ya mapendo daima, asubuhi mpaka jioni ya maisha yetu. Kukosa mafuta ndiyo ulegevu na usingizi usioisha mbele ya Neno la Mungu, mbele ya wajibu wangu katika familia, katika serkali, na maisha ya kila siku kwa ujumla. Ni kuacha kuweka nguvu katika kutafiti kwa unyenyekevu na kugundua mpango wa Mungu kwa njia ya alama za nyakati, na hivi kujiimarisha katika mambo ya dunia bila kuweka chachu ya injili.

Tunaweza kusema kuwa Mathayo anatutaka kuweka himizo kali katika maisha ya kila siku, yaani kuiona kila dakika ni ya maana katika kuandaa ujio wa pili wa Bwana ambao Kanisa latambua kuwa uko tayari kwa namna ya Ekaristi Takatifu ambamo Kristu huja daima. Sauti ya maskini, waliotengwa, na machozi ya wagonjwa ni sauti ya mchumba wa Kanisa Yesu Kristu ambaye daima kila siku anaita na Kanisa linaitika sauti hiyo kwa unyenyekevu katika utume wake.

Baada ya haya yote Mwinjili anatukumbusha mwishoni akisema angalieni mlango usije ukafungwa na ikatoka sauti ikisema siwajui ninyi! Kumbe yafaa sasa kushika lile fundisho la Bwana lisemalo “basi kesheni, kwa sababu hamjui siku wala saa”, Tumsifu Yesu Kristu.

Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.