2014-11-05 09:28:08

Rais JK. achonga na wazee wa Dodoma kuhusu masuala nyeti ya kitaifa!


Ifuatayo ni hotuba ya Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania, wakati akizungumza na wazee wa Dodoma, Jumanne tarehe 4 Novemba 2014 kuhusu masuala mbali mbali ya kitaifa na kimataifa!

Ndugu Wananchi;
Nakushukuru sana Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Dodoma, Mheshimiwa Balozi Job Lusinde kwa kuandaa mkutano huu. Wakati nilipofanya ziara ya Mkoa wa Dodoma tulipanga tukutane lakini kwa vile ratiba yangu iliingiliwa na mambo mengi, hivyo haikuwezekana, lakini leo imewezekana. Pengine hii ndiyo siku ambayo Mwenyezi Mungu alipanga tukutane.

Tumshukuru Muumba wetu kwa rehema zake, na tumuombe ajaalie mkutano wetu uanze salama na uishe salama. Nawashukuru kwa Risala yenu na maudhui yake. Nawaahidi nitayafuatilia na majibu mtapata. Pamoja na yaliyomo kwenye risala yenu mimi nina mambo manne ambayo ni yatokanayo na ziara yangu nchini China na Vietnam, maradhi ya Ebola, uchaguzi wa Serikali za Mitaa na hatua zinazofuata kwenye Mchakato wa Katiba.

Ziara ya China na Vietnam
Ndugu Wananchi;
Kuanzia tarehe 21 Oktoba, 2014 hadi tarehe 28 Oktoba, 2014 nilikuwa katika ziara rasmi ya kutembelea nchi za China na Vietnam. Nilitembelea China tarehe 21 hadi 26 Oktoba, 2014 na Vietnam tarehe 26 hadi 28 Oktoba, 2014. Ziara hizo nilizifanya kufuatia mwaliko wa Rais wa China, Mheshimiwa Xi Jinping na mwaliko wa Rais wa Vietnam Mhe. Truong Tan Sang. Ziara katika nchi hizo zilikuwa za mafanikio makubwa sana hata kuliko nilivyotarajia. Nchini China tulipokelewa kwa namna hawajafanya kwa miaka mingi.

Ziara ya China
Ndugu Wananchi;
Nchini China, kwa makubaliano na wenyeji wetu tulifanya hafla maalum ya kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China. Katika hafla hii upande wa China uliwakilishwa na Makamu wa Rais Mheshimiwa Li Yuanchao. Pande zetu mbili ziliitumia fursa hiyo kuzungumzia tulipotoka, tulipo sasa na mbele tuendako.

Kwa jumla wote tumeridhika kuwa tumekuwa na nusu karne ya uhusiano wenye mafanikio makubwa. Katika kipindi hiki nchi zetu zimekuwa marafiki wa kweli, wa kuaminiana na kusaidiana kwa mambo mengi. Katika medani za kimataifa nchi zetu zimekuwa zikielewana kwa mambo mengi na kusaidiana. China ilikuwa ngome kuu katika kusaidia kwa hali na mali harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika.

Wakati ule Tanzania ilikuwa ikiongoza nchi za mstari wa mbele. Wenzetu bado wanakumbuka sana jinsi nchi yetu ilivyokuwa mstari wa mbele kuipigania nchi ya China kurejeshewa haki yao hususan ya kuketi kiti chao katika Umoja wa Mataifa, baada ya Chama cha Kikomunisti chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mao Tse Tung kufanikiwa kukishinda Chama cha Kuomintang na kiongozi wake Chian Kai Sheki na kulazimika kukimbilia Taiwan. Mataifa makubwa ya Magharibi yalikataa kuitambua China mpya na kuitenga. Katika kufanya hivyo, waliitambua Taiwan na kuifanya kuwa ndiyo wawakilishi wa China katika Umoja wa Mataifa.

Baada ya hapo Jamhuri ya Watu wa China ilipinga uamuzi ule na kuanzisha kampeni ya kudai haki yake stahiki. Madai yao hayo yalipata nguvu pale Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere alipoamua kuwa Tanzania ishiriki katika kampeni hiyo kwa nguvu zake zote. Kwa kushirikiana na nchi nyingine rafiki, jitihada hizo za pamoja zilizaa matunda na mwaka 1971, China ilipokubaliwa kuchukua nafasi yake stahiki katika Umoja wa Mataifa na Taiwan kuondolewa.

Ndugu zetu wa China hawasahau msaada wetu huo na hawaoni haya kulisemea waziwazi jambo hilo na vizazi vyote vya China vinafundishwa kuhusu wema ambao Tanzania imewafanyia. Kwa sababu hiyo, Tanzania ina nafasi maalum nchini China. Wao wenyewe wana msemo maalumu kuhusu Tanzania kwamba ni “all weather friends”. Yaani marafiki wa majira yote.

Katika ziara yangu nilifuatana na kaka yangu Dkt. Salim Ahmed Salim ambaye ndiye alikuwa Balozi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa wakati ule. Rafiki zetu wa China walifurahi sana kumwona Dkt. Salim kwani yeye hasa ndiye aliyefanya kazi ya kushawishi nchi nyingine kuiunga mkono Jamhuri ya Watu wa China. Pia nilifuatana na Mheshimiwa Balozi Mstaafu Jenerali Mrisho Sarakikya aliyekuwa Mkuu wa Majeshi wa kwanza wa Tanzania. Yeye ndiye alihusika sana kujenga uhusiano wa mambo ya kijeshi baina ya nchi yetu na China. Pia, nilikwenda na Balozi Mstaafu, Mzee Waziri Juma aliyewahi kuwa Balozi wa Pili wa Tanzania nchini China.

Kama mjuavyo nchi ya China imetusaidia mambo mengi kwa maendeleo yetu. Misaada mingine ilihusu vitu vikubwa ambavyo katika hali ya kawaida isingewezekana kusaidiwa na nchi nyingine zinazotoa misaada ya maendeleo na mikopo. Miongoni mwa hayo ni ujenzi wa Reli ya Uhuru (TAZARA), misaada ya zana, vifaa na mafunzo vilivyosaidia kujenga Jeshi letu jipya yaani JWTZ baada ya kuvunjwa kwa lile tulilorithi kutoka kwa Wakoloni kuaasi Januari 20, 1964. Msaada wao mkubwa ndiyo uliotuwezesha mpaka kuweza kulinda na kukomboa nchi yetu dhidi ya uvamizi na kutekwa eneo la Misenyi, Kagera na majeshi ya dikteta Iddi Amin wa Uganda.

Hata sasa China imeendelea kuwa mshirika wetu mkubwa kuliko wote katika kuimarisha na kuendeleza Jeshi letu. Msaada mwingine mkubwa ni ule mkopo wa dola za Marekani bilioni 1.2wa kujenga bomba jipya la gesi kutoka Mtwara na Songosongo hadi Dar es Salaam. Isingekuwa rahisi kupata mkopo mkubwa kiasi kile kutoka nchi nyingine au Shirika lolote la fedha duniani. Mkopo ule unalimaliza tatizo la upungufu wa umeme kutokea sasa mpaka mwaka 2020 inapokadiriwa kuwa nchi yetu itahitaji megawati 10,000. Hata wakati huo bomba hili ni muundombinu wa msingi utakaorahisisha upanuzi wa miundombinu ya kuzalisha umeme kutosheleza mahitaji hayo kama itaamuliwa gesi iendelee kuwa chanzo kikuu cha nishati ya umeme nchini.

Katika mazungumzo yangu na Waziri Mkuu Li Keqiang na Rais Xi Jinping wote wawili wameelezea kuridhika kwao na uhusiano baina ya nchi zetu tangu siku za nyuma mpaka hapa tulipo sasa. Hali kadhalika walielezea kuwa wangependa kuona uhusiano wetu na ushirikiano wetu unaimarika na kukua mpaka kufikia hatua bora na ya juu kabisa. Niliwahakikishia kuwa hiyo ndiyo fikra yangu na Watanzania kuhusu uhusiano baina ya nchi zetu mbili rafiki.

Kwa nyakati tofauti viongozi wote wakuu wa China walinihakikishia utayari wao wa kuendelea kuchangia maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiusalama ya Tanzania. Jambo lililonipa faraja kubwa mimi na wenzangu ni kuwa mambo yote tuliyoomba ndugu zetu wa China watusaidie wamekubali. Hakika Wachina wameendelea kuwa marafiki wa kweli wa nchi yetu na watu wake.

Tuliwaomba waendelee kushirikiana nasi na wabia wenzetu wa Zambia kulijenga upya Shirika la Reli ya TAZARA na wamekubali. Tuliwaomba pia tuendelee kushirikiana kukuza uwekezaji na biashara baina ya nchi zetu mbili rafiki. Walilipokea jambo hilo kwa furaha. Ni ukweli ulio wazi kwamba biashara na uwekezaji umekua sana kiasi cha kuifanya China kuwa nchi inayoongoza kwa mambo yote mawili. Hata hivyo, sote tumekubaliana kuwa biashara ya dola za Marekani bilioni 3.7 na uwekezaji wa dola za Marekani bilioni 2.5 ni kidogo mno hivyo tuongeze juhudi tufanye vizuri zaidi katika kipindi kifupi kijacho.

Ndugu Wananchi;
Kulikuwa na mkutano mkubwa wa uwekezaji uliohudhuriwa na makampuni ya kichina yapatayo 500 yaliyokuwa tayari kuwekeza na kufanya biashara na Watanzania. Kwa upande wetu miradi kadhaa tuliyopeleka imepata wabia. Miongoni mwa waliofaninikiwa sana ni Shirika la Nyumba la Taifa waliopata wabia watakaowekeza dola za Marekani bilioni 1.7 kwenye ujenzi wa nyumba.

Aidha, kuhusu ujenzi wa Ukanda wa Kiuchumi wa Mbegani ambao tuliwaomba watusaidie kusukuma utekelezaji wake, viongozi wa China walielezea utayari wao kusaidia mradi huo ufanikiwe. Tulipokuwa Shenzhen, tulipata nafasi ya kutembelea Makao Makuu ya Kampuni ya China Merchants Ltd., na kuzungumza na viongozi wake. Walitembezwa kuangalia shughuli za kampuni hiyo ikiwa ni pamoja na jinsi Kampuni hiyo ilivyoshiriki katika ujenzi wa mji wa Shenzhen kutoka kijiji cha uvuvi na kuwa jiji kubwa la kisasa, lenye maendeleo ya kiuchumi, teknolojia na biashara. Waliahidi kutumia ujuzi wao, maarifa yao na uwezo wao wa kifedha kujenga Mbegani kama ilivyotokea Shenzhen.

Siku ile pia tulishuhudia Mfuko wa Akiba wa Oman wakitiliana saini na China Merchants na Mamlaka yetu ya Uendeshaji wa Maeneo Huru ya Uwekezaji (EPZA) hati ya makubaliano kujiunga rasmi katika kuwekeza na kushiriki katika utekelezaji wa mradi huo. Kilichonifurahisha sana siku ile ni kule kuwepo kwa mpango kazi unaotarajia ujenzi wa bandari na ukanda wa maendeleo ya kiuchumi wa Mbegani kuanza tarehe 1 Julai, 2015.

Hali kadhalika, nilipokuwa Shenzhen nilipata nafasi ya kutembelea kampuni za teknolojia ya habari na mawasiliano za Huawei na ZTE. Nilifika mjini Jinan, Jimbo la Shandong na kutembelea kampuni nyingine kubwa ya aina hiyo iitwayo INSPUR. Bahati nzuri kampuni zote zimewekeza Tanzania na wanataka kupanua uwekezaji wao.

Nilipokuwa Jinan nilitembelea Hospitali Kuu ya Jimbo la Shandgon, Mjini Jinan, ambayo imetoa madakatari wengi na kupata nafasi ya kuwashakuru viongozi wa Jinan na Jimbo la Shandong kwa kutuletea madakatari na wataalamu wengine wa afya kuja kufanya kazi nchini Tanzania. Vile vile, nimewashukuru kwa mchango wao muhimu uliotuwezesha kupata hospitali ya moyo katika Hospitali ya Muhimbili. Pamoja na kuwashukuru niliomba idadi iongezwe kwani mahitaji yapo na watu wanawapenda Madaktari wa China.

Yapo mambo mengi mazuri yaliyofanyika katika ziara yangu nchini China ambayo tutakesha kama tutahitaji kuyafafanua moja baada ya jingine. Hata hivyo, napenda kuyazungumzia mambo mawili. Kwanza ni taarifa aliyonipa Rais Xi Jinping kwamba wanaongeza ufadhili wa masomo kwa kutupa nafasi 100 zaidi kwa vijana wa Tanzania kusoma China kwa kipindi cha miaka mitano. Pia wamekubali kutusaidia ujenzi wa chuo cha ufundi (VETA) cha Mkoa wa Kagera. Aidha, wamekubali ombi langu la kuongeza idadi ya madaktari na wataalamu wa afya kutoka China kuja kufanya kazi nchini.

Ziara Vietnam
Ndugu Wananchi;
Baada ya kumaliza ziara yangu China nilitembelea Vietnam kwa siku mbili. Huko nako nilikwenda kuimarisha na kuendeleza uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi zetu, na kujifunza zaidi kutoka kwa wenzetu ambao wamepata mafanikio makubwa kiuchumi katika kilimo na viwanda kwa kipindi kifupi. Hii ni nchi ambayo tulianza nayo mageuzi ya kiuchumi wakati mmoja mwaka 1986. Wenzetu wameweza kupata mafanikio makubwa katika kilimo, viwanda, ufugaji wa samaki na mengine mengi. Kwa upande wa teknolojia ya mawasiliano ya simu, wanayo kampuni ya Viettel ambayo imekuwa kubwa duniani na inakusudia kuwekeza nchini.

Kwa kweli mafanikio ambayo Vietnam imepata tangu mwaka 1986 yanatupa matumaini kwamba na sisi Tanzania tunaweza kufanikiwa kama wao. Hatuna budi kujipanga vizuri. Tumekubaliana kushirikiana zaidi hasa kubadilishana uzoefu na maarifa katika kilimo na viwanda.

Ugonjwa wa Ebola
Ndugu Wananchi;
Jambo la pili ninalotaka kulizungumzia, si mara yangu ya kwanza kufanya hivyo. Hili si jingine bali ni tahadhari juu ya maradhi ya Ebola yaliyoanzia huko Afrika Magharibi katika nchi za Liberia, Sierra Leone na Guinea. Baadae yalifika Nigeria, Senegal, Mali, Marekani, Spain na Uingereza. Inakadiriwa kuwa ugonjwa huu hatari umekwishaua watu 4,960 na wengine 13,567 wameambukizwa toka ulipoanza hadi sasa. Ugonjwa huu umeendelea kuwa tishio la dunia kutokana na kasi kubwa ya kuenea kwake. Lakini hasa kwamba asilimia 70 mpaka 90 wanaoupata ugonjwa huu hupoteza maisha. Bahati mbaya hauna dawa wala kinga. Bado wataalamu wa dawa wanachuna bongo.

Taarifa njema ni kuwa ugonjwa huu haujaingia nchini Tanzania. Hata hivyo, hii haiondoi ukweli kuwa unaweza kufika kwani watu wanatembea kutoka nchi zenye maradhi haya na kuja nchini kwetu. Hapa jirani na sisi upo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Sitashangaa pia kwamba wapo Watanzania wanaokwenda nchi zenye maambukizi makubwa hata wakati huu. Watu hao wana hatari kubwa ya kupata maambukizi.

Narudia kukumbusha umuhimu wa kuchukua tahadhari kitaifa na kila mtu anayeishi hapa nchini. Sisi Serikalini tunaendelea kuchukua hatua stahiki na kuimarisha jitihada na hatua za kuwachunguza wageni katika mipaka yetu ya usafiri wa nchi kavu na usafiri wa anga. Tumejiandaa vya kutosha kutambua watu wenye joto kubwa zaidi ya joto la kawaida la mwili wa mwanadamu.

Hali kadhalika, tumewataka watu wanaoingia nchini kueleza kama katika wiki tatu zilizopita wametembelea nchi za Guinea, Sierra Leone na Liberia. Nia ya kutaka waseme siyo kuwazuia wasiingie nchini bali kuwapa ushauri juu ya dalili za ugonjwa wa Ebola na nini wafanye iwapo dalili hizo zitawatokea. Pia tunapenda kujua mahala watakapofikia ili tuweze kuwafuatilia.

Ndugu Wananchi;
Ninawaomba ushirikiano wa kila mmoja wenu kutoa taarifa kwa wakati mara mtakapoona mtu mwenye dalili za ugonjwa huo ambazo ni homa kali ya ghafla, kutokwa na damu mwilini, kutapika na kuharisha kwa wakati mmoja. Toeni taarifa ili wataalamu wenye ujuzi na vifaa stahili vya kujikinga waweze kuja kuwahudumia ipasavyo wagonjwa wenye dalili hizo. Jiepusheni na kumsogelea au kugusana na mtu wa aina hiyo. Na, maiti aliyekufa kutokana na ugonjwa wenye dalili hizo pia asiguswe. Kufanya hivyo ni kujiweka kwenye hatari ya moja kwa moja ya kuambukizwa kwani huenda mtu huyo ni muathirika wa Ebola. Toa taarifa upate maelekezo ya kitaalamu.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa

Ndugu Wananchi;
Kama mnavyofahamu tarehe 14 Desemba, 2014 tutafanya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji. Tumelazimika kufanya Uchaguzi huo mwezi Desemba, 2014 badala ya mwezi Oktoba kama ilivyostahili kutokana na shughuli za Bunge Maalum la Katiba kuendelea hadi tarehe 4 Oktoba, 2014 kwa kupitisha Katiba Inayopendekezwa. Kutokana na Taifa kuwa katika jambo lile kubwa ilionekana ni busara kuacha kwanza mchakato ule ukamilike kabla ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Nimeambiwa na TAMISEMI kwamba maandalizi ya uchaguzi huo yanakwenda vizuri na kwamba ratiba imekwishatolewa, na majina ya mitaa, vijiji na vitongoji vipya nayo yamekwishatolewa. Kazi ya kuandikisha wapiga kura itafanyika kuanzia tarehe 23 Novemba, 2014 na itamalizika kwa orodha ya wapiga kura kubandikwa mahali pa wazi hasa kwenye mbao za matangazo katika vitongoji, mitaa, na vijiji husika ifikapo tarehe 30 Novemba, 2014.

Kufanya hivyo kutawezesha wananchi kukagua orodha hiyo kuona kama majina yao yapo, na kujiridhisha kuwa majina ya wale walioandikishwa kwenye daftari hilo ni wapiga kura wenye sifa stahiki za kupiga kura katika uchaguzi huo katika eneo husika. Nawasihi wananchi wote mjitokeze kwa wingi kujiandikisha na kukagua orodha ya wapiga kura itakapobandikwa ili kufanikisha zoezi hilo.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi vyama vya siasa vinapaswa kuwasilisha fomu za wagombea wao kwa Msimamizi wa Uchaguzi kuanzia tarehe 20 hadi 22 Novemba, 2014. Kwa maana hiyo, wale wenye shauku, nia na sifa za kugombea uongozi katika uchaguzi ujao wa Serikali za Mitaa, wanapaswa kutega sikio ili kujua ratiba za uchaguzi na uteuzi ndani ya vyama vyao ili wapate fursa ya kuteuliwa kugombea.

Napenda kuchukua fursa hii kuwahimiza wananchi wote wakiwa pia vijana na wanawake wasibakie nyuma, wajitokeze kwa wingi kugombea nafasi hizo na nyingine katika Uchaguzi Mkuu ujao. Ratiba ya uchaguzi huo iliyotolewa na TAMISEMI inaonyesha kwamba mikutano ya kampeni ya kuwanadi wagombea itafanyika kwa siku 14 kuanzia tarehe 30 Novemba, 2014 hadi tarehe 13 Desemba, 2014 siku moja kabla ya siku ya kufanyika kwa uchaguzi huo.

Ndugu Wananchi;
Mfumo wa utawala wa nchi yetu huanzia katika ngazi ya kitongoji na mtaa kisha kijiji, kata na hatimaye taifa. Kwa hiyo uchaguzi wa vitongoji, mitaa na vijiji ndiyo msingi wa uongozi na utawala wa nchi yetu. Tukipata viongozi wazuri katika ngazi hii ya msingi, tutakuwa tumefanikiwa sana katika kuimarisha utawala bora na kuongeza kasi ya maendeleo yetu. Rai yangu kwenu, wananchi wenzangu ni kuwa mjitokeze kwa wingi wakati wa kampeni kuwasikiliza wagombea wetu wakijieleza, kisha tuwachague wale watu ambao sisi tunaona wanatufaa. Lazima tutambue kuwa ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji ndiyo msingi wa uongozi wa nchi yetu. Tukipata watu wazuri tutakuwa tumejenga msingi imara wa uongozi katika taifa letu.

Watu wote watakaojitokeza kugombea katika ngazi ya vitongoji, mitaa na vijiji vyetu ni watu tunaoishi nao na kwamba tunawafahamu vizuri sana. Hatuna budi kuvitendea haki vijiji, mitaa na vitongoji vyetu kwa kuwachagua viongozi wazuri watakaokuwa chachu ya maendeleo katika maeneo yetu. Tukifanya makosa ya kuchagua watu wasiofaa tuelewe kwamba tutakuwa tumejinyima fursa ya kuwa na viongozi bora kwa kipindi cha miaka 5 ijayo. Pia tunaweza kuzua migogoro na kupunguza kasi ya maendeleo katika maeneo yetu. Tusione haya kuwashawishi watu wazuri wajitokeze kugombea.

Mchakato wa Katiba na Kura ya Maoni

Ndugu wananchi,
Bunge la Katiba lilikamilisha kazi yake ya kutunga Katiba mpya ilipofika tarehe 2 Oktoba, 2014 ambayo ilikuwa siku mbili kabla ya muda uliopangwa wa tarehe 4 Oktoba, 2014. Tarehe 8 Oktoba, 2014, Mwenyekiti wa Tume ya Katiba aliikabidhi Katiba hiyo kwangu na kwa Rais wa Zanzibar kama yalivyo matakwa ya Kifungu cha 28A(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba. Kwa mara nyingine tena nawapongeza kwa dhati aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Mhe. Samuel John Sitta, Makamu wake Mhe. Samia Suluhu na Wajumbe wa Bunge Maalum la Katiba kwa kazi kubwa na nzuri. Wametupatia Katiba Inayopendekezwa inayojitosheleza kwa kila hali. Nawapongeza pia Makatibu wa Bunge, Sekretarieti yao na wafanya kazi wote. Bunge Maalum la Katiba linastahili pongezi nyingi kwa kazi nzuri waliyofanya na hasa kwa kuikamilisha ndani ya muda wa uliopangwa wa siku 130 tu. Baadhi ya nchi duniani jukumu hili limechukua muda mrefu zaidi ya uliokusudiwa au hata kushindikana.

Tutakuwa wachoyo wa fadhila tusipoipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba chini ya uongozi wa Mwenyekiti Mheshimiwa Jaji Joseph Sinde Warioba na Makamu wake Mheshimiwa Jaji Augustino Ramadhani pamoja na Wajumbe wote wa Tume hiyo. Tunawapongeza kwa kutayarisha Rasimu nzuri ya Katiba ambayo ndiyo iliyoliongoza Bunge Maalum la Katiba kupata Katiba Inayopendekezwa iliyo bora. Kilichobakia ni kuwaachia wananchi kuamua kama wanaitaka Katiba Inayopendekezwa au hapana. Watafanya hivyo kwenye kura ya maoni itakayofanyika kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba na Sheria ya Kura ya Maoni iliyotungwa kutekeleza matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Ndugu wananchi,
Miaka ya nyuma kulikuwa na tangazo la sabuni ya Omo lililokuwa likisema “Uzuri wa Ngoma Sharti Uicheze”. Uzuri wa Katiba Inayopendekezwa siyo wa kuambiwa. Unahitaji uione, uisome na uielewe. Imeandikwa kwa Kiswahili rahisi na fasaha. Inasomeka na kueleweka kwa urahisi sana. Ni rai yangu kwamba wananchi wote muipate nakala ya Katiba Inayopendekezwa na mjisomee. Sheria imeniagiza kuichapisha Katiba hiyo kwenye gazeti la Serikali ndani ya siku saba baada ya kukabidhiwa. Nimekwisha kufanya hivyo. Aidha, Sheria inaeleza kwamba Katiba Inayopendekezwa isambazwe kwenye magazeti ya kawaida ndani ya siku 14. Zoezi hili ni endelevu. Usambazaji wa Katiba Inayopendekezwa unaendelea na utaendelea mpaka Kura ya Maoni itakapopigwa.

Wito wangu kwenu Watanzania wenzangu ni kwamba msikubali kulaghaiwa na maneno ya wale wachache wanaotaka kuturudisha nyuma na kutunyima fursa ya kupata Katiba iliyo bora zaidi. Maana hapajawahi kutokea ushiriki mpana kama huu katika kutengeneza Katiba katika nchi yetu. Pengine, hata kwingineko duniani si wengi wametoa fursa kama tulivyofanya sisi.

Kura ya Maoni
Ndugu wananchi,
Sheria ya Kura ya Maoni iliniagiza kutangaza tarehe ya Kura ya Maoni katika Gazeti la Serikali ndani ya siku 14 baada ya kupokea Katiba Inayopendekezwa. Nimefanya hivyo. Awali Sheria hiyo iliagiza Kura ya Maoni ifanyike na matokeo yake yajulikane ndani ya siku 70. Waziri mwenye dhamana ya Uchaguzi alipowauliza viongozi wa Tume ya Uchaguzi kuhusu utekelezaji wa matakwa hayo ya Sheria, Tume ilisema isingweza kuendesha Kura ya Maoni ndani ya muda huo. Mambo yanayohitajika ni mengi mno ambayo hayawezi kukamilika katika muda huo. Wakaomba wapewe muda zaidi. Bahati nzuri Kifungu 51 cha Sheria ya Kura ya Maoni kimetoa mamlaka kwa Waziri mwenye dhamana ya Uchaguzi baada ya kushauriana na Waziri anayehusika na Uchaguzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kubadilisha masharti haya kama kutakuwa na umuhimu wa kufanya hivyo.

Baada ya mashauriano hayo, Mawaziri wenye dhamana ya uchaguzi wa pande zetu mbili za Muungano waliridhika kuwa upo umuhimu wa kusogeza mbele muda ili kutoa fursa kwa Tume kukamilisha taratibu inazowajibika kufanya. Hayo ni pamoja na kuboresha Daftari la Kudumu la Mpiga Kura, matayarisho ya upigaji wa Kura ya Maoni na mambo mengine kadhaa.

Hivyo basi, tarehe 03 Oktoba, 2014, Waziri mwenye dhamana ambaye ni Waziri Mkuu kwa kutumia mamlaka aliyopewa ya Kifungu cha 51 cha Sheria ya Kura ya Maoni, alitangaza kupitia gazeti la Serikali kubadilisha sharti la siku 70 na kuacha Rais aamue siku ya kupiga kura. Kwa sababu ya mabadilikio hayo, tarehe 10 Oktoba, 2014 nilitangaza kupitia Gazeti la Serikali kuwa Kura ya Maoni itakuwa tarehe 30 Aprili, 2015 ili kutoa fursa kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kukamilisha taratibu zake. Katika tangazo hilo pia, nilielekeza kuwa kampeni zitaanza tarehe 30 Machi na kuisha tarehe 29 Aprili, 2014 siku moja kabla ya siku ya kupiga kura, kama ilivyo desturi yetu katika upigaji kura hapa nchini.

Ndugu Wananchi;
Natambua kuwepo dhana kuwa siku za kampeni ni 60. La hasha! Siku za Kampeni zinaamuliwa na Rais, kufuatia Kifungu cha 4 (2) b kisemacho: “Amri kwa ajili ya kura ya maoni itakuwa kama ilivyo kwenye fomu iliyotajwa kwenye jedwali la Sheria hii, na itaainisha:
(a) Katiba Inayopendekezwa kuandikwa;
(b) Kipindi ambacho kampeni kwa ajili ya Kura ya Maoni itafanyika;
(c) Kipindi ambacho Kura ya Maoni itafanyika”

Tume ya Uchaguzi ina mamlaka ya kuruhusu vyama vya kijamii na vya kiraia kutoa elimu ya umma ndani ya siku 60 kabla ya siku ya Kura ya Maoni. Tume imepewa mamlaka hayo na Kifungu cha 5 (4) cha Sheria ya Kura ya Maoni. Kwa sababu hiyo, nawaomba Watanzania wenzangu tuzingatie matakwa ya Sheria ya Maoni ambayo imeelekeza vizuri kuhusu lini Kura ya Maoni itafanyika na lini wadau watoe elimu kwa umma. Naomba tuwe na subira mpaka hapo Tume ya Uchaguzi itakapotoa maelekezo ya utekelezaji wa fursa husika kwa wadau.

Ndugu wananchi,
Ni matarajio yangu kwamba wananchi wote mtajitokeza kwa wingi kwenda kuboresha taarifa zenu kwenye Daftari la Kudumu la Mpiga Kura kama itakavyoelekezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, na hatimaye itakapofika tarehe 30 Aprili, 2015 mtakwenda kwa wingi kupiga kura ya kuamua kuhusu hatma ya Katiba Inayopendekezwa. Naomba mfanye uamuzi mzuri. Fursa hii ni adhimu na ya kihistoria ambayo tukiipoteza huenda itachukua miaka mingi kuipata tena. Mtakapokuwa mnakwenda kupiga kura zingatieni maslahi yenu pamoja na ya watoto na wajukuu zenu, maana Katiba ndiyo inayoweka misingi na mstakabali wa taifa letu sasa na karne nyingine zijazo.

Hitimisho
Ndugu Watanzania wenzangu,
Naomba nimalizie kwa kuwasihi mjitokeze kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika tarehe 14 Desemba, 2014. Endeleeni kusoma Katiba Inayopendekezwa ili muda utakapofika kila mtu atoe uamuzi stahiki na wenye maslahi kwa nchi yetu. Nimezitaka Wizara na Taasisi zinazohusika na utekelezaji wa makubaliano yetu na Serikali ya China na Vietnam kuchukua hatua za ufuataliaji na wanipe taarifa. Narudia kutoa wito tuendelee kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa Ebola. Nawaomba muendelee kuiunga mkono Serikali yetu katika jitihada zake za kuiletea maendeleo nchi yetu na watu wake.

Mwisho, ingawa siyo kwa umuhimu, vijana wetu 297,488 wameanza mtihani wa taifa wa kidato cha nne jana tarehe 3 Novemba, 2014. Tuna imani wamejiandaa vya kutosha na wameandaliwa vyema na walimu, wazazi na walezi wao kwa ajili ya mtihani huo. Naungana na walimu, wazazi, walezi na Watanzania wote kuwatakia kila la heri katika mtihani wao huo.

Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Ahsanteni Sana kwa kunisikiliza!








All the contents on this site are copyrighted ©.