2014-11-05 08:46:50

Kanuni msingi za mawasiliano katika mitandao ya kijamii!


Askofu Josè Ignacio Munilla Aguirre, Rais wa Tume ya Mawasiliano ya Jamii, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, CCEE, hivi karibuni, akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la wakurugenzi wa habari kutoka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya amegusia mambo makuu manne, yanayoweza kutumiwa na Mama Kanisa ili kuwasiliana kwa ukamilifu zaidi na walimwengu, mintarafu changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya Mawasiliano Duniani kwa Mwaka 2014.

Jambo la kwanza ni muda ambao ambao unavifanya vyombo vya mawasiliano ya jamii kuchanganyikiwa kwa kutaka kuwafikia watu wengi kwa mkupuo na kwa haraka zaidi, kiasi hata cha kupoteza ukweli na maana ya ujumbe uliokuwa unakusudiwa. Waandishi wa habari hawana muda wa kuzama zaidi katika kutafuta ukweli na matokeo yake wanatoa habari nyepesi nyepesi zisizokuwa na uzito mkubwa unaokusudiwa.

Jambo la pili ni kuhakikisha kwamba, umoja unapewa kipaumbele cha kwanza katika habari badala ya kujikita katika kinzani na migawanyo inayosababisha adha na machungu katika maisha ya watu. Wakristo hawana budi kujitahidi kuwa kweli ni vyombo vya haki, amani na upatanisho; dhana inayojengwa na kuimarishwa katika utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini; kuamua kwa kuzingatia imani na ukweli. Ushuhuda wa Kikristo unajikita katika sadaka na majitoleo kwa wengine na wala si wingi wa maneno.

Jambo la tatu anasema Askofu Aguirre, Wakristo wanapaswa kusimamia ukweli utakaowaweka huru hata kama una gharama zake badala ya kubaki wanaelea katika ombwe kwa mawazo ya kufikirika. Mawazo yaendane na ukweli ili kuepukana na kinzani zinazoweza kujitokeza katika masuala haya. Kumbe, Wakristo wajitahidi kutangaza ukweli unaofumbatwa katika upendo.

Jambo la nne ili kuwawezesha Wakristo kufanya mawasiliano bora zaidi ni kuwa na matumizi sahihi ya utandawazi katika sekta ya mawasiliano pamoja na kuzingatia tunu msingi za maisha ya watu bila ya kubeza yale mambo msingi yanayopatikana ndani ya jamii husika; daima mafao ya wengi yapewe kipaumbele cha kwanza. Kanuni hizi zikipata mwelekeo mpana ni muhimu sana.

Akichangia mada katika mkutano huu, Padre Antonio Spadaro, Mkurugenzi mkuu wa Jarida la "Civiltà Catolica" anabainisha kwamba, ni vigumu kuweza kuzungumzia kuhusu shughuli za kichungaji na mawasiliano pasi ya kukazia tunu msingi za maisha ya kiroho.

Mitandao ya kijamii ni jukwaa ambamo watu wanamwilisha tunu msingi za maisha ya kijamii, kiroho na kiutu. Ni uwanja unaogusa maisha ya watu kila siku. Hapa ni mahali ambapo, waamini na watu wenye mapenzi mema wanaweza kushirikishana tunu msingi za Kiinjili na kwamba, waamini wanaweza kutumia jukwaa hili kwa ajili ya kuwamegea jirani zao imani yao kwa Kristo na Kanisa lake.







All the contents on this site are copyrighted ©.