Kwa mara ya kwanza katika historia ya maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu, Sinodi maalum
kwa ajili ya Familia imekuwa na mvuto, changamoto na tafakari za kina, kwani maisha
ya ndoa na familia ni mambo yanayowagusa wote, kila mtu kwa kadiri ya nafasi na dhamana
yake ndani ya Jamii. Baba Mtakatifu Francisko ameshiriki kikamilifu katika maadhimisho
ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia iliyofunguliwa hapo tarehe 5 hadi
tarehe 19 Oktoba 2014.
Baba Mtakatifu
aliguswa na mchango wa Mababa wa Sinodi iliyokuwa inatolewa kwa kuzingatia: ukweli,
uwazi, uzoefu na mang’amuzi ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia sehemu
mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu wakati wote ameonesha hali ya utulivu, huku akisikiliza
kwa makini na kuhimiza ukweli na uwazi, mambo msingi yatakayoliwezesha Kanisa kuibua
mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya familia, wakati wa maadhimisho
ya Sinodi ya kawaida ya Maaskofu itakayofanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 4 hadi
tarehe 25 Oktoba 2015.
Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anabainisha
kwamba, maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia ni hija ndefu
ambayo itafanyika kwa kipindi cha miaka miwili, kwani ni “Sinodi nyeti” inayogusa
masuala tete yanayojikita katika Sheria za Kanisa na Mafundisho tanzu ya Kanisa. NI
Sinodi inayogusa maisha na utume wa Kanisa kwa kuwashirikisha kwa namna ya pekee kabisa
waamini walei, pamoja na viongozi wa Kanisa; ili kwa pamoja waweze kupata dira na
mwelekeo wa maisha ya kichungaji kwa ajili ya familia. Hapa Kanisa linataka kutembea
kwa kuendelea kutangaza Injili ya Familia, kama walivyofanya Mababa wa Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican. Kuna matatizo, changamoto na fursa ambazo Mama Kanisa, anapaswa
kuzifanyia kazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia.
Padre Lombardi
anasema, maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia
yalianza kwa kutuma maswali dodoso kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema; Baba
Mtakatifu akaitisha mkutano maalum wa Makardinali ili kujadili kuhusu utume wa Kanisa
kwa ajili ya familia na hatimaye, Mabaraza ya Maaskofu Kikanda na Kitaifa yakapata
fursa ya kujadili na mwishoe, Hati ya Kutendea kazi kwa ajili ya Mababa wa Sinodi
ikatolewa.
Sinodi ambayo maana yake ni kutembea kwa pamoja, imewashirikisha
watu wengi ili kupata mwelekeo wa shughuli za kichungaji kwa kujikita katika Mafundisho
Tanzu ya Kanisa. Kila jambo lilifanyika kadiri ya mpango wa Kanisa na wala hakuna
kitu ambacho kilitolewa kwa kushtukiza.
Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri
na hotuba yake ya ufunguzi wakati wa maadhimisho ya Sinodi, aliwataka Mababa wa Sinodi
kuzunguza kwa kuzingatia ukweli na uwazi; uhuru pasi na wasi wasi, kama misingi madhubuti
ya mchakato wa majadiliano ya Sinodi. Wakati wote alikaa kimya na kuwasikiliza Mababa
wa Sinodi wakijadili na mwishoni, akawashirikisha uzoefu na mang’amuzi yake wakati
wa maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya familia, kwa kuiwezesha Sinodi
kubaki katika mwelekeo wake wa kiimani, tayari kuwatangazia Watu wa Mataifa Injili
ya Familia.
Baba Mtakatifu alikuwa ni mhimili mkuu wa umoja na mshikamano
wakati wote wa maadhimisho ya Sinodi, ameonesha utulivu wa ndani hata pale ambapo
watu walidhani kwamba, Kanisa linameguka. Ajiweka chini ya usimamizi na maongozi ya
Roho Mtakatifu, kwa ajili ya mafao na ustawi wa Kanisa la Kristo. Ameliwezesha Kanisa
kufanya mang’amuzi ya kina, ili Kanisa liweze kupata mwelekeo sahihi kwa ajili ya
Injili ya Familia.
Padre Lombardi anasema, Hati Elekezi kutoka kwa Mababa
wa Sinodi ilipata mwangwi mkubwa kutoka kwenye vyombo mbali mbali vya habari, lakini
kwa masikitiko makubwa, baadhi ya vyombo hivi vilipotosha ukweli kwa ajili ya mafao
yao binafsi. Majadiliano ya Mababa wa Sinodi katika makundi madogo madogo yameweza
kuboresha hati elekezi na hatimaye kupata Hati ya Sinodi ambayo Baba Mtakatifu Francisko
amekabidhiwa tayari kutumwa kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki kama hati ya majadiliano.
Vyombo
vingi vya mawasiliano ya jamii vilijikita katika mada ya wanandoa walioachana na baadaye
kuamua kuoa au kuolewa tena na uwezekano wa kushiriki katika Sakramenti za Kanisa
pamoja na swala tete la ndoa za watu wa jinsia moja, lililopigiwa debe kiasi hata
cha “kutibua nyongo” miongoni mwa Familia ya Mungu. Lakini watu wameweza kufahamishwa
kwa kina na mapana yale yaliyojadiliwa na Mababa wa Sinodi.
Padre Lombardi
anasema, Sinodi hii imeliwezesha Kanisa kutembea kwa pamoja ili kutafuta mapenzi ya
Mungu minaytafu mwanga wa Injili na Imani ili kuibua mikakati itakayoliwezesha Kanisa
kuihudumia Familia kwa kusoma alama za nyakati. NI matumaini ya Padre Lombardi kwamba,
Familia ya Mungu itaweza sasa kushiriki kikamilifu tena ili kuweza kupata mwelekeo
mpya katika maadhimisho ya Awamu ya Pili ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia.
Imehaririwa
na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.