Novena kwa ajili ya kuombea haki, amani na upatanisho Burkina Faso
Kardinali Philippe Nakellentuba Ouèdraogo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ouagadougou,
Burkina Faso, anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema nchini Burkina Faso
kuungana kwa pamoja ili kusali kwa ajili ya kuombea haki, amani na utulivu katika
kipindi hiki kigumu cha historia ya nchi yao, baada ya nguvu ya umma kumlazimisha
Rais Blaise Compaorè, tarehe 30 Oktoba 2014 kutema ngazi na kukimbilia uhamishoni
Pwani ya Pembe, baada ya jitihada za kutaka kubadili Katiba ya nchi kushindikana.
Kwa sasa Serikali ya mpito inaongozwa na Jeshi, chini ya Luteni Kanali Isaac
Zida, moja ya askari kikosi cha ulinzi wa Rais. Serikali ya mpito inasema, itarudia
utawala wa kiraia mapema iwezekanavyo, lakini vyama vya upinzani vinataka utawala
wa kiraia kuongoza nchi na wala si kuendekeza tena masuala ya mapinduzi ya kijeshi
ambayo yameligharimu sana Bara la Afrika!
Waamini nchini Burkina Faso tangu
tarehe 2 hadi tarehe 9 Novemba 2014 wanasali kwa ajili ya kuombea upatanisho wa kitaifa,
haki na amani nchini Burkina Faso. Kardinali ametunga sala maalum akimwomba Mwenyezi
Mungu awasaidie watunga sheria hekima na busara itakayohakikisha ustawi na maendeleo;
uhuru, haki na amani kwa wananchi wote wa Burkina Faso.