Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha,
kilichoko mjini Vatican, Jumanne tarehe 4 Novemba 2014 anasema kwamba, sheria inayoongoza
Ufalme wa Mungu inawataka watu kujitoa bila ya kujibakiza, lakini kutokana na ubinafsi,
uchu wa mali na madaraka, watu wengi wameshindwa kuupokea mwaliko huu, kwa kushindwa
kuonesha imani kwa Mwenyezi Mungu.
Baba Mtakatifu akifanya rejea kwenye Injili
ya Siku anakazia kwamba, watu wengi waliakwa, lakini kila mmoja alitoa sababu za kukataa
kushiriki mwaliko huu kutokana na: Ubinafsi, kiburi, majivuno na hali ya mtu kujisikia
na wala hawakutaka kupoteza muda na shughuli zao za uzalishaji; mambo ambayo yanalaumiwa
na Yesu mwenyewe kwani ni mwaliko uliokuwa unajikita katika majitoleo binafsi, bila
hata ya kujibakiza kidogo.
Yesu anaendelea hata kiasi cha kuwahimiza wafuasi
wake kusikiliza sauti ya Mungu inayowaalika kila siku ya maisha yao na kuitikia kwa
moyo wa dhati bila kumgeuzia Mwenyezi Mungu kisogo, mambo ambayo wakati mwingine yanasababisha
mateso na mahangaiko kwa Wakristo kama ilivyokuwa kwa Wafuasi wa Emmau au kwa Mtakatifu
Tomma aliyetaka kugusa madonda ya Yesu, ili apate kuamini. Mwenyezi Mungu anawaalika
waja wake ili kushiriki katika karamu yake, lakini kwa bahati mbaya watu bado wanaonesha
shingo ngumu, kwa kuendelea kuogelea katika dimbwi la dhambi, mapungufu ya kibinadamu
bila kufanya maamuzi magumu ya kutoka nje ili kushirikiana na wengine, hali ambayo
inawadumaza.
Baba Mtakatifu anasema kuna wakati ambapo Mwenyezi Mungu anawalazimisha
waja wake kushiriki katika karamu yake, kama inavyojionesha katika Injili ya siku
na kwamba, ni kwa njia ya majaribu mengi, watu wanaweza kufanya maamuzi mazito katika
maisha yao, ya kujitoa bila ya kujibakiza, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu ni
kielelezo makini cha majitoleo haya, kwani anamkirimia mwanadamu ukombozi hata pasipo
mastahili yake.
Baba Mtakatifu anasema, utakatifu wa maisha na wokovu ni zawadi
kutoka kwa Mungu inayopokelewa kwa mtu kujisadaka mwenyewe, kama Yesu alivyofanya
katika maisha yake; kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake. Msalaba uwe ni tiketi
ya kuingilia katika karamu ya uzima wa milele, hata kama mwamini anaelemewa na mapungufu
yake, jambo la msingi ni kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu bila kuogopa, bali kufungua
malango ya mioyo na kutenda kadiri ya uwezo uwezo wake, kwani karamu inaandaliwa na
Mwenyezi Mungu mwenyewe!