2014-11-04 08:16:52

Mshikamano wa Baba Mtakatifu kwa wananchi wanaoteseka huko Mashariki ya Kati!


Askofu mkuu Giovanni Pietro Dal Toso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa linaloratibu misaada ya Kanisa Katoliki, Cor Unum baada ya ziara yake ya kikazi nchini Syria anasema, hali bado ni tete kwa wananchi wengi wa Syria baada ya vita kuendelea kurindima nchini humo kwa miaka mitatu sasa. Kanisa litaendelea kuonesha mshikamano wa upendo kwa wote wanaoteseka kutokana na vita pamoja na kinzani za kijamii kwa kushirikiana na Kanisa mahalia katika kuwahudumia watu kwa hali na mali.

Akiwa nchini Syria, Askofu mkuu Dal Toso, amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na viongozi mbali mbali wanaoratibu misaada kwa ajili ya wananchi wa Syria. Ameshiriki pia katika mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Syria ambao wameiomba Jumuiya ya Kimataifa kusitisha kabisa biashara ya silaha kwa Syria kwani ni chanzo cha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Maaskofu wamewataka pia Wakristo kushinda kishawishi cha kutaka kukimbia kutoka huko Mashariki ya Kati.

Askofu mkuu Dal Toso anasema, hadi sasa kuna jumla ya wakimbizi na wahamiaji millioni kumi kutoka Syria wanaohitaji msaada wa dharura, kwani ni watu ambao wameathirika kwa kiasi kikubwa na madhara ya vita na kinzani za kijamii. Kuna umati mkubwa wa watu ambao hauna fursa za ajira; watu wanaendelea kutumbukizwa katika umaskini wa hali na kipato pamoja na magonjwa; shule zinashindwa kutoa elimu kwa kuhofia usalama wa maisha ya wanafunzi, jambo ambalo ni hatari kwa kizazi kijacho.

Askofu mkuu Dal Toso anasema, ziara yake ya kikazi nchini Syria ililenga pamoja na mambo mengine kuonesha mshikamano na Kanisa mahalia pamoja na kuwatia shime Mashirika ya misaada, ili yaendelee kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji kwa ari na moyo mkuu pasi ya kukata tamaa. Cor Unum imeliwezesha Kanisa nchini Syria kuwahudumia watu zaidi ya millioni moja na nusu wanaoishi huko Syria, Lebanon, Yordani na Uturuki.

Wananchi kwa namna ya pekee, wanamshukuru Baba Mtakatifu Francisko na Kanisa kwa ujumla kwa kuonesha mshikamano wa upendo katika shida na mahangaiko yao ya kila siku. Wanapenda kutoa mwaliko kwa pande zote zinazohusika kuanza tena mchakato wa majadiliano na upatanisho wa kitaifa, ili amani na utulivu viweze kurejea tena nchini Syria.







All the contents on this site are copyrighted ©.