2014-11-03 07:41:07

Walengwa wakuu wa mashambulizi ya kigaidi ya Boko Haram ni Wakristo!


Jimbo Katoliki la Maiduguri, Nigeria ni kati ya Majimbo ambayo yameathirika vibaya sana kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, ambacho kinaendelea kutishia usalama na maisha ya wananchi wengi wa Nigeria. Jimbo la Maiduguri ambalo liko Kaskazini mwa Nigeria, limepata hasara ya Makanisa yake 185 kuchomwa moto na kwamba, zaidi ya watu 190, 000 wamelazimika kuyakimbia makazi yao, ili kuokoa maisha yao kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara.

Boko Haram kwa sasa inaendelea kushikilia maeneo mengi Kaskazini mwa Nigeria kana kwamba, Serikali imekwenda likizo. Viongozi wa Kanisa wanasema, Boko Haram inashikilia miji 25 iliyoko Kaskazini mwa Nigeria. Watu wengi wananyimwa uhuru wa kuabudu, demokrasia na kwamba, haki msingi za binadamu ziko hatarini kupokwa na Kikundi cha Boko Haram.

Ikumbukwe kwamba, kuna wazee, watoto na wanawake ambao hawana uwezo wa kukimbia, hivyo wanalazimika kubaki majumbani mwao; makundi haya ya watu yako hatarini. Wanawake wanaokamatwa na Boko Haram wanatekwa na kubakwa na wakati mwingine wanalazimishwa kuolewa na wanajeshi wa Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, unyama unaotendeka mbele ya Jumuiya ya Kimataifa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria hivi karibuni katika mkutano wao wa mwaka wametamka wazi wazi kwamba, kutokana na mashambulizi yanayofanywa na Kikundi cha kigaidi cha Boko Haram na makundi mengine ya kigaidi, Nigeria iko hatarini, changamoto kwa Serikali kuhakikisha kwamba, inalivalia njuga tatizo hili ambalo kwa sasa linaonekana kuwa ni “janga la kitaifa”.

Amani, utulivu, ustawi na maendeleo ya wengi ni mambo msingi na wala si watu kuanza kufikiria kuhusu uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika nchini Nigeria, mwaka 2015. Ingawa hata Waamini wa dini ya Kiislam wanaguswa wakati wa mashambulizi yanayofanywa na Boko Haram, lakini walengwa ni Wakristo na waamini wa dini nyingine.

Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria, kwa kuguswa na mahangaiko na mateso kwa watu walioathirika kutokana na mashambulizi ya kigaidi yanayofanywa na Boko Haram, wameamua kwamba, tarehe 13 na 14 Novemba 2014, watasali pamoja, ili kuombea umoja na mshikamano wa kitaifa, ili kuokoa maisha ya watu wanaoendelea kumwaga damu yao pasi na hatia.








All the contents on this site are copyrighted ©.