Viongozi wachovu na walevi wa madaraka wamekumbana na nguvu ya umma nchini Burkina
Faso!
Baraza la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linasema, machafuko ya kisiasa nchini humo
ni matokeo ya kukithiri kwa rushwa na ufisadi uliokuwa unafanywa na baadhi ya wanasiasa
wasiokuwa na uzalendo wala machungu ya mahangaiko ya watu wao. Haya pia ni maendeleo
ya sayansi na teknolojia ya habari ambayo inatumiwa na vijana wengi katika mchakato
wa kuhabarishana, katika misingi ya ukweli na uwazi. Vijana wengi wamechoshwa na hali
inayoendelea nchini mwao na hivyo kwa sasa viongozi wa kisiasa wanaiona nguvu ya umma.
Maaskofu
Katoliki Burkina Faso wanasema, tangu mwaka 1985 idadi ya watu wasiojua kusoma wala
kuandika imeongezeka maradufu kutoka asilimia 16. 17% hadi kufikia asilimia 32%. Katika
miaka ya hivi karibuni kumekuwepo na maendeleo makubwa ya vyombo vya mawasiliano ya
kijamii, kiasi kwamba, watu wanapata habari nyingi, ikilinganishwa na miaka kadhaa
iliyopita. Maaskofu wanasema hapa kuna maendeleo ya vitu lakini watu wanaendelea kuogelea
katika dimbwi la umaskini wa hali na kipato na kwamba, pengo kati ya maskini na matajiri
linazidi kuongezeka maradufu.
Utajiri wa nchi unamilikiwa na kundi la watu
wachache hali ambayo imesababisha manung'uniko miongoni mwa raia wa Burkina Faso.
Kundi hili wanasema Maaskofu limekuwa na nguvu kubwa ya kifedha kiasi kwamba, wakati
huu rushwa inatembezwa wazi wazi na kwamba, ubadhirifu wa mali ya umma umefikia kiwango
cha hali ya juu kabisa.
Baadhi ya viongozi wa kisiasa wameanza kulewa madaraka
kiasi hata cha kutaka kupindua Katiba ya nchi kutokana na uchu wa madaraka, matokeo
yake wanasiasa wachovu wamekiona cha mtema kuni kwa kukumbana na nguvu ya umma. Baraza
la Maaskofu Katoliki Burkina Faso linawataka wananchi kutulizana na kudumisha amani
na usalama wakati huu wa kipindi cha mabadiliko!