Mpendwa Msikilizaji wa Kipindi chetu cha Kanisa la nyumbani, Tumsifu Yesu Kristo!
Karibu katika kipindi chetu pendevu tuendelee kupyaishana juu ya yale yaliyojiri katika
Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.
Lengo letu:
Mtaguso utue vizuri katika familia na maisha yako, ili tuuishi katika maisha yetu
ya kila siku. Miongozo ya Mtaguso ndiyo dira ya kufuata ili sote kama waana wa Kanisa
twende pamoja. Jumuiya yoyote ile ya watu isiyokuwa na miongozo thabiti, hukosa mwelekeo
na mwisho huwa ni kambi ya fujo. Ili kulipatia Kanisa mwelekeo sahihi kwa nyakati
mbalimbali, Mamlaka halali ya Kanisa na kwa utaratibu maalumu, hutupatia miongozo
ya kuifuata ili tuweze kufikia lengo. Haswaa, ndiyo ilivyokuwa kwa Mtaguso mkuu wa
Pili wa Vatican. Ndiyo maana mpendwa msikilizaji, tunakumbushana kile tulichoagizwa,
ili nyakati zetu hizi zenye kelele nyingi, tusipoteze mwelekeo. Twende pamoja, tukafike
salama bandarini pa Yesu. Leo “tuidonoe” kwa umbali, hati ya Mwanga wa Mataifa
ambayo ni Katiba. Hati hiyo juu ya Kanisa ndiyo muhimu kuliko nyingine zote za mtaguso,
ndiyo maana tunakuta imesheheni mambo mengi hata yale yaliyomo katika hati nyinginezo
pia. Inajibu swali la Mwenyeheri Papa PauloVI, lililouliza, “Kanisa, unasemaje juu
yako?”. Katika hati hii, Kanisa linajieleza, linajifafanua, linajidhihirisha undani
wake na utume wake na nafasi yake zaidi katika Ukombozi wa Mwanadamu.
Sura
ya kwanza inafafanua fumbo la Kanisa kama sakramenti. Kwa nje linaonekana katika muundo
wa jamii ya watu na kwa ndani limebeba neema zisizoonekana kwa macho. Ndani ya Kanisa
Mungu anaishi na kufanya kazi. Na ndiyo maana twasema kwa njia ya Kanisa tunapata
neema, kwa sababu Kanisa ni chombo cha neema za Mungu. Tunaelezwa pia jinsi Baba,
Mwana na Roho Mtakatifu wanavyohusika na Kanisa. Hati hii inalieleza Kanisa kama kundi
la kondoo, shamba, jengo na hekalu la Mungu au bibiarusi anayeungana na Bwanaarusi
wake kuwa mwili mmoja, yaani mwili wa Kristo. Wazee wetu wa Mtaguso walitumia lugha
za picha ili kutusaidia sisi kuelewa zaidi fumbo la Kanisa.
Sura ya pili inaeleza
jinsi watu wanavyohusika na fumbo la Kanisa. Kwa njia ya sakramenti sote tumefanywa
kuwa taifa mmoja la Mungu. jinsi ambavyo katika Agano la Kale Mungu mwenyewe aliliridhia
kuwaokoa watu kama taifa na siyo mtu mmoja mmoja, hali kadhalika sasa Mungu anatuokoa
sote kwa njia ya Kanisa kama taifa lake takatifu. Katika taifa hilo watu wote wanapaswa
kuingia bila ya ubaguzi ili wawe kitu kimoja. Ndiyo maana linaitwa katoliki, yaani
la watu wote, wa mahali pote na nyakati zote.
Pamoja na mafundisho hayo, yapo
pia mafundisho mengine yanayoleta uzito katika sura nzima ya Kanisa katika muundo
wale na katika Imani yake. Kuna mafundisho kuhusu muundo wa uongozi wa Kanisa, hasa
uaskofu. Tunafundishwa kwamba kama vile mitume walivyokuwa kundi moja na Petro akiwa
kiongozi wao, maaskofu wote pia ni kundi moja (kwa sababu ndiyo warithi wa mitume)
na Askofu wa Roma yaani Baba Mtakatifu, mrithi wa Mtume Petro na wakili wake Yesu
Mwenyewe, ndiyo Kiongozi na Mkuu wa Maaskofu hao na Kanisa zima. Mtaguso huu, umesisitiza
pia umoja wa maaskofu, ukielekeza kila mmoja wao afanye kazi yake akishirikiana na
kundi lote la waamini na achangie ustawi wa Kanisa zima, si jimbo lake tu. Kinachosisitizwa
hapa ni umoja na ushirikiano katika uongozi wa Kanisa, na pia kumtazama jirani pia.
Ubinafsi ni aina ya uchoyo mharibifu.
Sehemu hii ndiyo inafungua dirisha kwa
Kanisa letu la nyumbani yaani familia. Kama tulivyosikia na tutaendelea kusikia tena
na tena, Familia ni Kanisa la Nyumbani. Ili kanisa hilo dogo la nyumbani liweze kustawi
vema, linahitaji miongozo na uongozi thabiti. Miamba mikuu miwili ya usitawi wa Kanisa
la nyumbani ni Baba na Mama. Na ili Baba na Mama ambao wameungana kwa wito maalumu
wa ndoa waweze kutimiza wajibu wao vizuri, wanahitaji kuwa na Umoja wenye upamoja
na ushirikiano kati yao. Baba na Mama wajitahiti kuwa na kauli mmoja kwa maslahi na
usitawi wa familia. Inapotokea kwamba baba na mama wamegawanyika, hawasikilizani katika
masuala ya msingi ya familia, hapo wajue wazi kuwa wanaligawanya Kanisa la nyumbani.
Jinsi ambavyo Mtaguso unasisitiza umoja kati ya Askofu na Kanisa analolisimamia,
na sisi leo tunataka kusisitiza sana umoja kati ya wazazi na watoto, umoja ndani
ya familia. Usitawi wa familia huwa hauletwi tu na fanaka za mali na vipaji walivyonavyo
wanafamilia. Roho ile ya umoja, ndiyo inayojenga familia. Na umoja wa kweli uliyositawi
ndani ya familia, huwa na matunda mema kwa jirani. Familia yetu inaponeemeka na kusitawi
sana, tusisahau kuwa sisi ni sehemu ya mwili wa fumbo wa Kristo kama walivyo na familia
nyinginezo pia. Hivi kama familia tuna wito pia wa kuchangia amani na usitawi wa familia
nyinginezo, kwa sala, ushauri mwema na matendo ya upendo. Haileti furaha kwetu kama
sisi wanafamili tunafikiri kuwa tunaishi kwa amani na starehe zinazokaribiana na anasa,
na wakati familia zote zinazotuzunguka wanapiga miayo mirefu ya njaa na magonjwa na
kila adha. Umoja na usitawi wetu, utukumbushe kumtazama jirani. Jirani akisitawi,
sisi kama familia tutafurahi zaidi na tutakuwa na amani zaidi.
Nyakati zetu
hizi, pamoja na mambo mengine mengi, mchwa mbaya sana unaotafuna familia nyingi ni
mtengano na ukorofi-katiri uliyopo katika ya baba na mama. Wazazi kama viongozi wa
familia, wakikikosa umoja tu, hata watoto pia watakosa umoja. Kwa lazima, watatokea
watoto wa baba, na watoto wa mama. Baba atalazimisha watoto wamchukie mama yao na
mama atalazimisha watoto wamchukie baba yao.
Mwishoni mwa siku, familia nzima
inakuwa sio kanisa la nyumbani tena bali ni sumu kwa majirani na sumu kwa Kanisa zima.
Inakuwa ni kambi ya kuunda watu wenye hasira, wakali na waliojikatia tamaa. Katika
hali hiyo, hata shughuli za uzalishaji mali pia zitakosa unadhifu kwa sababu kutakuwa
na miradi ya baba na miradi ya mama. Hakuna miradi ya familia, kisa? Wazazi wamekosa
umoja. Hatimaye mali hizo inakuwa ni mwendelezo wa fujo zaidi ndani ya familia.
Kumbe
mpendwa msikilizaji, tunapotafakari juu ya hadhi ya Kanisa na Muundo wa Kanisa mintarafu
uongozi, tusisahau kujiuliza na kujielekeza maswali haya: Tunataka familia yetu iwe
ya namna gani. Swali hili linajibiwa na wanafamilia wote. Na baada ya hapo, sisi kama
familia, utume wetu kwa familia majirani ni upi? Tunafanya nini katika kuchangia usitawi
wa familia za wenzetu? Endapo tutajikuta kama familia tumepindapinda kidogo, basi
tujipe ujasiri, tuitishe mtaguso wa kifamilia, ili tujitambue, tujikosoe, tujipe maana
chanya zaidi na mwelekeo mzuri. Kwa njia hiyo tutakuwa kweli tunashikiri fumbo na
utume wa Kanisa na papo hapo kama Kanisa lilivyo Mwanga kwa Mataifa, familia yetu
nayo itakuwa Nuru kwa majirani wote. Na iwe hivyo!! Kutoka katika Studio za Radio
Vatican, ni mimi Padre Pambo Martin Mkorwe OSB.