2014-11-03 12:20:24

Mambo yanayokwamisha ustawi wa Kanisa ni mashindano yasiyokuwa na tija na majivuno!


Mashindano na majivuno ni sumu kali katika maisha na utume wa Kanisa, changamoto na mwaliko kwa waamini kujikita katika roho ya umoja, unyenyekevu na mapatano, daima mafao, ustawi na maendeleo ya Kanisa yakipewa kipaumbele cha kwanza, bila ya mtu kujitafuta mwenyewe! Umoja na mshikamano ndani ya Kanisa ni matunda ya Roho Mtakatifu, mwaliko kwa waamini kushiriki sehemu yao. Mtakatifu Paulo anawaalika waamini kutoshindana wala kutafuta utukufu wa mtu binafsi wala kujikweza; mambo ambayo bado yanajionesha hata kwa watu wa nyakati hizi.

Ni sehemu ya mahubiri ya Baba Mtakatifu Francisko aliyoyatoa Jumatatu asubuhi tarehe 3 Novemba 2014, kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican, kwa kuwataka Wakristo kujivika moyo wa unyenyekevu, umoja na mshikamano, ili kuliimarisha Kanisa, kama alivyofanya Mtakatifu Martin De Porres ambaye Mama Kanisa amefanya kumbu kumbu yake siku ya Jumatatu. Ni Mtawa aliyejikita katika tasaufi ya huduma na moyo wa unyenyekevu, daima akajitahidi kutafuta mafao ya wengi.

Baba Mtakatifu anasema, hii ndiyo furaha inayopaswa kuoneshwa na Askofu, anapoona Kanisa linastawi katika upendo, umoja na unyenyekevu bila ya kuwadharau wengine kuwa "si mali kitu"! Inasikitisha kuona kwamba, hata ndani ya Kanisa na taasisi zake, kuna baadhi ya watu wanaoweka mbele masilahi yao binafsi badala ya huduma na mapendo. Ni mwaliko wa kuchunguza dhamiri na kuona ikiwa kama Kanisa na taasisi zake kwa ujumla zinatekeleza dhamana na wajibu wake kadiri ya changamoto zilizotolewa na Liturujia ya Neno la Mungu?







All the contents on this site are copyrighted ©.