Bwana, tufundishe kusali, Lk. 11:1-4. Ni kauli iliyotolewa na Mitume wa Yesu baada
ya kumwona akisali kwa umakini mkubwa, kiasi cha kuacha mvuto na chapa katika hija
ya maisha yao ya kiroho.
Wataalam
wa masuala ya maisha ya kiroho wanabainisha kwamba, mtu anayefahamu kusali vyema,
ana uwezo wa kuwafundisha wengine kusali vizuri zaidi, kwani ni mtu aliyefundwa, akafundika
katika kujenga na kuimarisha mahusiano na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zake. Hivi
ndivyo ilivyokuwa kwa Yohane Mbatizaji, lakini zaidi kwa Yesu Mwenyewe!
Mtu
wa sala au mchamungu anatambua fika kwamba, sala ni nguzo ya maisha inayomwezesha
mwamini kujenga mahusiano thabiti na Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zake. Huu ni
utambuzi kwamba, daima Mwenyezi Mungu yuko tayari kusikiliza sauti na kilio cha waja
wake, wakati wote wanapomkimbilia kwa imani na matumaini. Huu ndio urithi mkubwa ambao
Yesu Kristo amewaachia wafuasi wake katika hija ya maisha yao ya kiroho, baada ya
kumwona anasali kwa umakini mkubwa, tofauti kabisa na walimu wengine waliokuwepo nyakati
hizo.
Sala makini inahitaji maandalizi ya dhati, kwani sala ni sanaa; ni sayansi,
ni utambuzi, lakini zaidi ya yote ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwa ajili
ya wengine. Sala ni nguvu ya ndani na wala si wingi wa maneno. Ni mwelekeo wa kutambua
kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba mwema, mwingi wa huruma na mapendo. Kwa mwamini anayependa
kusali kwa dhati kabisa anapaswa kuwa na imani thabiti sanjari na kuonesha utii, ili
kuimarisha mahusiano yake na Mungu pamoja na jirani zake, walioumbwa kwa sura na mfano
wa Mungu.
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio
Vatican.