Katiba mpya itawasaidia kuchuchumilia utakatifu wa maisha!
Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kimissionari na Kazi za Kitume, limepitisha Katiba
ya Shirika la Wafuasi wa Yesu, hapo tarehe 16 Oktoba 2014. Shirika linapenda kuchukua
fursa hii kuwapongeza kwa namna ya pekee Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, Papa
Francisko, Kardinali Velasio De Paolis na washauri wake walioliwezesha Shirika kufikia
hatua hii baada ya kupitia katika kipindi cha giza na hali tete katika maisha na utume
wake.
Katiba Mpya ya Shirika inafumbata kanuni msingi zinazopania kulinda na
kudumisha karama ya Shirika pamoja na kuiendeleza. Hayo yamebainishwa na Padre Eduardo
Robles-Gil, Mkuu wa Shirika la Wafuasi wa Yesu. Katiba hii inatekeleza kwa dhati mambo
msingi ambayo yalibainishwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika mchakato
wa kulipyaisha Shirika, ulioanza kunako mwaka 2010 kwa kumteua Kardinali Velasio De
Paolis kuwa msimamzi wa kipapa, dhamana iliyoendelezwa na Baba Mtakatifu Francisko
alipoingia madarakani.
Katiba mpya ni matunda ya kazi ya miaka mitatu iliyofanywa
kwa njia ya sala na tafakari ya kina, kwa kuwashirikisha wanashirika wote katika hatua
mbali mbali na hatimaye, kuitishwa kwa mkutano mkuu wa Shirika uliohitimisha rasmi
dhamana ya Kardinali De Paolis, mkutano ambao uliadhimishwa kati ya Mwezi Januari
na Februari 2014.
Katiba hii inalenga kuwasaidia anasema Padre Eduardo Robles-Gil
wanashirika kuchuchumilia utakatifu wa maisha sanjari na kutekeleza utume wao ndani
ya Kanisa, kwa kuwahudumia Watu wa Mungu, mintarafu maisha ya kitawa miongoni mwa
Wafuasi wa Yesu.