2014-10-31 08:12:44

Tanzania kujenga maghala makubwa katika mikoa sita na ujenzi wa bandari ya Bagamoyo kuanza Julai 2015!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Serikali inalenga kujenga maghala kwenye mikoa sita kupitia mkopo ambao itaupata kutoka Serikali ya Poland ili kuhifadhi chakula kabla ya kununuliwa na Serikali. Jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Bagamoyo linatarajiwa kuwekwa Julai, 2015.

Waziri mkuu Pinda ameyasema hayo wakati kizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Alhamisi, Oktoba 30, 2014 mara baada ya kuwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Mwl. Julius Nyerere akitokea Oman. Waziri Mkuu alisema alikwenda Poland kutafuta msaada wa mfumo wa mkopo wenye masharti nafuu ambao utasaidia kupambana na tatizo la uhaba wa maghala kwa ajili ya kuhifadhia nafaka.

“Tumelenga mikoa sita ya kuanzia ambayo ni Ruvuma, Rukwa, Njombe (pamoja na Iringa) ambako kuna uzalishaji mkubwa wa mahindi. Pia tunaangalia Kanda ya Ziwa ambako mara nyingi wana uhaba wa chakula; tutaweka na Dodoma kwa sababu ni katikati ya nchi ili ikusanye akiba kutoka mikoa ya jirani ya Singida, Manyara na Tabora,” alisema.

“Eneo la mwisho ni Moshi kwa maana ya kukusanya mazao kutoka Arusha, Kilimanjaro na Tanga ili kukabiliana na uuzaji holela wa chakula nje ya mpaka wa nchi yetu,” alisema wakati akijibu maswali ya waandishi wa habari kwamba ni mikoa ipi itapewa kipaumbele katika zoezi hilo.

Alisema Serikali ya Poland imepanga kutoa Euro milioni 100 (sawa na sh. bilioni 240/-) ambazo alisema hazitoshi kukamilisha mahitaji yaliyopo nchini na kwamba Serikali inatarajia kuomba kiasi cha Euro milioni 500 (sawa na sh. trilioni 1.2/-) ili iweze kutimiza malengo yake.

“Mkopo wao ni wa riba ndogo mno kiasi cha asilimia 0.25 lakini jambo kubwa ni kwamba wameonyesha moyo wa kutusaidia katika eneo hili la chakula na wako tayari...,” alisema Waziri Mkuu. Alisema alikutana na wawekezaji na wafanyabiashara wa nchi hiyo ambao alisema wameonesha nia ya kuwekeza katika maeneo ya mifugo, kilimo, afya, maji na nishati. “Tumepata mwitikio mzuri na wameonyesha nia ya kuja hapa nchini mapema,” alisema.

Akijibu swali kuhusu muda ambao ujenzi huo utachukua ili kukabiliana na kilio cha wakulima, Waziri Mkuu alisema kulingana na teknolojia wanayotumia, haitazidi miezi mitatu hadi minne kabla ya ujenzi huo kuwa umekamilika.

“Lengo ni kupata uwezo wa kuhifadhi tani 700,000 hadi 1,000,000 na ujenzi wao siyo kama huu wa kwetu. Tumewaomba watujengee SILOS (maghala makubwa) kwa sababu zina teknolojia ya kujua kiasi gani cha nafaka kimeingia, zina unyevu kiasi gani, unaweza kuweka dawa nafaka zako, kuosha na kukausha na kisha ukasindika kwa kiwango unachotaka,” aliongeza Waziri Mkuu.

Alisema uzalishaji mwaka huu umetoa ziada ya tani milioni 1.5 za nafaka na tani 800,000 za mpunga ikilinganishwa na ziada ya tani 300,000 iliyokuwepo mwaka jana. “Serikali inakabiliwa na changamoto ya kupata soko la uhakika kwa mazao ya wakulima kwa sababu tulizoea kumtumia Wakala wa Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kama mnununzi mkuu na uwezo wezo wake ni tani 240,000 tu kwa mwaka,” alisema.

Akiwa Oman, Waziri Mkuu anasema walifikia makubaliano kwamba Ofisi ya Waziri Mkuu iendelee kuratibu maandalizi ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa bandari ya Bagamoyo utakaozishirikisha China na Oman yenyewe. “Tumekuabaliana jiwe la msingi la kuazna ujenzi liwekwe Julai mwakani,” alisema.

Waziri Mkuu alisema fursa kubwa iliyoko Oman ni uhakika wa soko la chakula kwa mazao yanayozalishwa hapa nchini na hasa mpunga. “Oman ina wakazi wapatao milioni nne, hana uwezo wa kutumia ardhi yake kuzalisha chakula kwa sababu ya jangwa. Kwa hiyo wanatumia kiasi cha dola za Marekani milioni 30 kununua chakula kila mwaka. Tunaweza kupata kiasi cha hela hizi tukiamua kuwauzia chakula,” alisema.

Mapema, Waziri Mkuu aliwaeleza waandishi hao kwamba, alitembelea nchi za Uingereza, Poland na Oman ambako alikutana na wafanyabiashara kwa nyakati tofauti na kuwaeleza fursa mbalimbali zilizoko nchini Tanzania lakini pia alikutana na Watanzania waishio Poland na Oman na kujibu maswali mbalimbali kutoka kwao.








All the contents on this site are copyrighted ©.