2014-10-31 11:26:26

Maisha ya wahamiaji na wakimbizi wengi yako mashakani!


Kardinali Antonio Maria Veglio', Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum anasikitika kusema kwamba, wahamiaji na wakimbizi wengi watakufa maji pasi na msaada huko baharini kutokana na uamuzi wa Serikali ya Italia kuacha kutoa huduma kwa wakimbizi na wahamiaji waliokuwa hatarini wakati wakijaribu kuvuka bahari kuingia Barani Ulaya. Kuanzia tarehe Mosi, Novemba, huduma hii inatolewa na Jumuiya ya Ulaya na unajulikana kwa jina la "Triton".

Huduma ya Triton imekabidhiwa meli sita, ndege mbili na elikopta moja kwa ajili ya huduma katika Bahari ya Mediterania, changamoto ambayo inapaswa kuvaliwa njuga na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ulaya, bila kutegeana, ili kuokoa maisha ya wahamiaji na wakimbizi wengi wanaotafuta nafasi ya kuingia Barani Ulaya

Kardinali Veglio' anasema kwamba, uhamiaji ni tatizo kubwa na lenye changamoto kibao kutokana na utete wake, kwani kuna makundi makubwa ya watu yanalazimika kuyakimbia makazi yao kwa kuhofia usalama wa maisha yao kutokana na: vita, njaa, umaskini; dhuluma na nyanyaso za kidini na hata wakati mwingine watu wanakimbia nchi zao kutokana na majanga asilia. Wakimbizi kutoka Syria, Iraq na Ethiopia wanaendelea kuongezeka siku hadi siku kutokana na hali halisi ilivyo katika nchi hizi.

Serikali ya Italia ilianza kutoa huduma ya kuokoa wahamiaji na wakimbizi baharini kunako tarehe 3 Oktoba 2013, wakati dunia iliposhuhudia watu 368 wakizama na kufa maji baharini. Licha ya jitihada hizi, bado kuna watu zaidi ya 300 wamefariki maji katika kipindi cha mwaka mzima uliopita, changamoto kwa Jumuiya ya KImataifa kuonesha moyo wa huruma na mshikamano kwa watu wanaotafuta hifadhi ili kuokoa maisha yao kutokana na majanga mbali mbali wanayokabiliana nayo.

Wakimbizi na wahamiaji hawa ni watu ambao wameonja suluba na mateso makali kabla ya kuchukua maamuzi machungu ya kupanda mashua huku wakifahamu fika kwamba, wanatembea na kifo machoni pao. Mwelekeo wa nchi mbali mbali za Ulaya kuziba masikio, kufunga macho na midomo yao ili kutosikiliza kilio na mahangaiko ya wahamiaji na wakimbizi wanaotafuta hifadhi ya maisha ni jambo la kusikitisha sana na kwamba, hiki ni kielelezo cha kumong'nyoka kwa utu na mshikamano kati ya watu. Ni utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko.

Wakimbizi na wahamiaji ni tatizo na changamoto endelevu katika maisha ya mwanadamu, jambo la msingi ni kwa watu kuelimishwa na kufahamishwa kuhusu changamoto hii ili kuifanyia kazi badala ya kuwafukuza na kuwataka warejee makwao ambako watakumbana na kifo uso kwa uso!







All the contents on this site are copyrighted ©.