Wananchi wa Burkina Faso, hivi karibuni wameandamana kupinga mabadiliko ya Katiba
yanayotaka kumpatia nafasi Rais Blaise Campaorè kuendelea kubaki madarakani hata baada
ya kumaliza muda wake wa kuongoza nchi kama Rais kwa awamu mbili kadiri ya Katiba
ya nchi. Zaidi ya watu millioni moja walijimwaga barabarani na hapo wakakumbana na
"mkono wa sheria", wakiwataka wanasiasa kuheshimu Katiba ya nchi ambayo kimsingi ni
sheria mama.
Ikiwa kama Bunge litafanikiwa kurekebisha Katiba ya Nchi ya Burkina
Faso, basi, Rais Campaorè atatinga tena kwenye kinyang'anyiro cha kuwania Urais kunako
mwaka 2015. Itakumbukwa kwamba, aliingia madarakani kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi
kunako mwaka 1987, baada ya Rais Thomas Sankara kuuwawa kikatili. Kwa kipindi cha
miaka kumi na minne ameongoza Serikali ya Burkina Faso.