2014-10-30 10:22:22

Uinjilishaji ni kiini cha maisha na utume wa Kanisa!


Kanisa ambayo kimsingi ni Sakramenti ya wokovu, linatumwa kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu, kama sehemu ya utii wa agizo lililotolewa na Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Dhamana hii kwa mara ya kwanza ilitekelezwa na Mitume, waliofuata nyayo za Yesu, wakahubiri Neno la uzima na kuanzisha Makanisa. Waandamizi wa Mitume wanao wajibu msingi wa kuhakikisha kwamba, Neno la Mungu linaendelea kutukuzwa, huku Ufalme wa Mungu ukitangazwa na kusimikwa duniani kote!

Amri ya kimissionari ya Bwana Yesu ina chanzo na kilele chake katika upendo wa milele unaopata chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kwa tabia yake, Kanisa linalosafiri hapa duniani ni la kimissionari, kwani linachota chanzo chake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ili kuwawezesha watu kushiriki katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Uinjilishaji ni kielelezo cha mapendo ya Mwenyezi Mungu kwa binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa watumiaji wa mitandao ya kijami anakumbusha kwamba, utume wa kwanza kabisa ndani ya Kanisa ni Uinjilishaji; ili kuwatangazia Watu wa Mataifa Habari Njema ya Wokovu!







All the contents on this site are copyrighted ©.