2014-10-30 07:32:00

Maendeleo ya kweli yazingatie mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili


Jumuiya ya Kimataifa ina wajibu wa kimaadili kulinda na kutetea haki msingi za watu mahalia, lakini kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa haki msingi za binadamu na uhuru wa kweli, ili kuwashirikisha kikamilifu katika mchakato wa maendeleo yanayozingatia mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Sera na mikakati ya maendeleo haina budi kuwahusisha watu mahalia, kwa kuheshimu utambulisho na tamaduni zao, bila ubaguzi.

Ni mchango uliotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Bernaditto Auza, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa wakati akichangia mada kwenye mkutano mkuu wa sitini na tisa wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa uliokuwa unajadili haki msingi za watu mahalia. Ujumbe wa Vatican unaunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali mbali mbali katika kufutilia mbali ubaguzi kwa kuhakikisha kwamba, watu mahalia wanashiriki kikamilifu katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya maendeleo yao.

Jumuiya ya Kimataifa haina budi kuhakikisha kwamba, utamaduni wa watu mahalia unalindwa na kuendelezwa, kwa kuheshimu tunu msingi za maisha ya watu zinazojikita katika zawadi ya maisha, utu na ushiriki wa watu katika masuala yanayowagusa kwa karibu zaidi bila kusahau ibada zao. Katika ulimwengu wa utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia pamoja na kuibuka kwa miji, tunu hizi msingi zinaweza kubezwa na hatimaye kuwekwa kando kama “gari bovu”.

Ujumbe wa Vatican katika mkutano huu, umekazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa kulinda na kuheshimu utu wa watu mahalia; haki ya kupata maendeleo ya kweli mintarafu utambulisho na tunu msingi za maisha pamoja na kushirikishwa katika kufanya na kutekeleza maamuzi mbali mbali. Hapa kuna haja ya kudumisha sheria zinazojikita katika haki; umiliki wa ardhi na utunzaji bora wa mazingira.








All the contents on this site are copyrighted ©.