2014-10-30 09:58:52

Kuna watoto wengi kutoka Eritrea wanaofariki dunia wakiwa njiani kwenda Ulaya!


Taarifa kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba, kuna kundi kubwa la watoto kutoka Eritrea wanaoingia Barani Ulaya bila ya usimamizi wa wazazi wao, lakini kwa bahati mbaya, hakuna taarifa rasmi zinazoonesha ni watoto wangapi wanaopoteza maisha yao wakiwa njiani kuelekea Barani Ulaya. Hadi kufikia kati kati ya mwezi Oktoba, 2014, zaidi ya watoto 4, 000 waliwasili nchini Italia kutoka Eritrea. Watoto hawa wanapaswa kupewa msaada pamoja na kulindwa!

Hayo yamebainishwa na Bi Sheila B. Keetharuth, mwakilishi maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Eritrea anayeshughulikia haki msingi za binadamu. Anasema, kuna watoto wanaokimbia kutoka katika familia, kambi za kijeshi na maeneo hatarishi, ili kusalimisha maisha yao bila ya ulinzi wala usimamizi wa wazazi wao, wakiwa na tumaini la kukutana na Wasamaria wema watakaowasaidia kupata haki zao msingi, lakini kwa bahati mbaya wakati mwingine wanatumbukia kwenye mikono ya wafanyabishara ya binadamu na hapo wanaendelea kuteseka na kunyanyasika utu na heshima yao.

Bi Keetharuth anasema kuna uvunjaji mkubwa wa haki msingi za binadamu nchini Eritrea ndo maana anaunga mkono uundwaji wa Tume itakayochunguza madai ya uvunjwaji wa haki msingi, ili wahusika waweze kufikishwa kwenye mkondo wa sheria. Wito unatolewa kwa wadau mbali mbali kuonesha ushirikiano wao wa dhati, ili tume hii iweze kukamilisha kazi yake.







All the contents on this site are copyrighted ©.