2014-10-30 07:16:12

"Fanyeni yote mapya katika umoja" Mahenge kumekucha!


Jimbo Katoliki Mahenge tarehe 30 Oktoba 2014 linaadhimisha kilele cha Jubilee ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kwa kuongozwa na kauli mbiu “Fanyeni yote mapya katika umoja”. RealAudioMP3

Katika maadhimisho haya anasema Askofu Agapiti Ndorobo, mkazo umewekwa kwa wanandoa waliokuwa wanaishi “uchumba sugu” kuhakikisha kwamba, wanarekebisha ndoa zao, mwaliko ambao umeonesha mafanikio makubwa Jimboni Mahenge kwa waamini kufunga na kubariki ndoa zao.

Katika maadhimisho haya, familia zimehimizwa kujenga na kudumisha: umoja, upendo na mshikamano wa dhati, kwa kutambua kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya sala na utakatifu wa maisha; hapa ni mahali pa toba na msamaha wa kweli. Wanaondoa wamehimizwa kusali kwa pamoja ili waweze kudumu katika maisha yao na utume wao wa kulea na kurithisha imani kwa watoto wao kama sehemu ya wajibu msingi wa wazazi.

Pale ambapo hakuna umoja, mshikamano na upendo wa dhati, matokeo yake ni watoto kuteseka na kuanza kuibuka kwa familia tenge na watoto wanaoishi katika mazingira magumu, changamoto kubwa katika malezi na makuzi ya watoto hawa ambao ni tegemeo la Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Ugumu wa maisha ya ndoa katika familia umejionesha hata katika malezi ya Kipadre na Kitawa, kumbe ili kupata Kanisa imara kuna haja kwa wanandoa kushikamana, kupendana na kusaidiana katika safari hii, huku wakichukuliana kwa imani, mapendo na matumaini anasema Askofu Agapito Ndorobo katika mahojiano maalum na Radio Vatican.

Katika kipindi cha miaka 50, Jimbo Katoliki Mahenge limeendelea kujielekeza katika mchakato wa kujitegemea kwa kuimarisha Halmashauri za Walei katika ngazi mbali mbali, ili kulitegemeza Kanisa kwa hali na mali pamoja na kuwasaidia Mapadre na wadau mbali mbali wa Uinjilishaji, ili waweze kutekeleza dhamana na utume wao kwa ari na moyo mkuu zaidi.

Katika kilele cha maadhimisho ya Jubilee ya Jimbo Katoliki Mahenge, Askofu Ndorobo anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kufanya yote mapya katika Kristo; kwa kujikita katika upendo, umoja na mshikamano wa dhati, ili kuleta mabadiliko na kuchochea maendeleo ya watu: kiroho na kimwili, hususan katika sekta ya elimu, afya na uchumi endelevu.

Askofu Ndorobo anatambua umuhimu wa Wakleri kama wasaidizi wake wakuu katika kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza Watu wa Mungu, Jimbo Katoliki Mahenge, anawaalika kufanya yote mapya katika Kristo kwa kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano katika kupanga na kutekeleza mikakati ya shughuli za kichungaji katika medani mbali mbali za maisha ya Familia ya Mungu, Jimboni Mahenge.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.